SHIRIKISHO la Soka barani Afrika (CAF) limesema hatua ya kuahirisha michuano ya CHAN kutoka mwezi ujao hadi Agosti inanuia kuyapa mataifa andalizi fursa ya kutosha kujipanga vyema kwa fainali hizo zitakazoshirikisha nchi 19 za Afrika.
Wadhamini wa mashindano hayo, TotalEnergies wamesema zawadi ya mshindi wa michuano hiyo imeongezwa kutoka Sh442 milioni, huku pesa zitakazogharimia zawadi kwa jumla zikifikia Sh1.3 bilioni.
Kwenye taarifa iliyotolewa Jumanne jioni, kamati kuu ya CAF ilisema ilipata ushauri kutoka kwa kamati yake ya wataalamu wa kiufundi waliosema kwamba mataifa ya waandalizi-Kenya, Uganda na Tanzania yanahitaji miezi kadhaa kulainisha kila kitu kwa ajili ya mashindano hayo ya wanasoka wanaosakia ligi za nyumbani.
“Mafanikio makubwa yamefanyika nchini Kenya, Uganda na Tanzania ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa viwanja vya kuchezea pamoja na vile vya kufanyia mazoezi, hoteli, hospitali, viwanja vya ndege pamoja na bidhaa nyingine muhimu kwa ajili ya fainali hizo, lakini tumeshauriwa na wataalamu wetu wa ufundi na miundombinu tuyasukume mbele kuhakikisha kila kitu kipo katika viwango vinavyohitajika ili kuandaa michuano itakayofana zaidi,” taarifa hiyo ilisema.
Ilisema wataalamu hao wa kiufundi ni miongoni mwa maafisa wa CAF ambao wamekuwa hapa nchini kuendelea kukagua shughuli za ujenzi zinazofanyika kwenye viwanja vilivyopendekezwa kwa ajili ya fainali hizo zilizopangwa kufanyika kuanzia Februari 1 hadi Februari 28.
Licha ya hatua hiyo ya kuahirisha michuano hiyo, Rais wa CAF Patrice Motsepe alipongeza mataifa hayo matatu kwa juhudi zao, huku akiwapongeza marais William Ruto wa Kenya, Samia Suluhu Hassan (Tanzania) na Yoweri Museveni wa Uganda kwa juhudi zao za kuhakikisha kila kitu kinakuwa tayari.
Kibali cha kuandaa CHAN kilitolewa Disemba 2023 kama kipimo kabla ya fainali za 2027 za AFCON ambazo pia zitaandaliwa kwa pamoja na mataifa hayo ya Afrika Mashariki.
Awali, mataifa 19 yalitarajiwa kushiriki katika mashindano hayo ya CHAN kabla ya Libya na Tunisia kujiondoa.
Mataifa yaliyothibitisha kushiriki ni Kenya, Uganda, Tanzania, Angola, Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo-Brazzavile, DR-Congo, Guinea, Madagasarm Mauritania, Morocco, Niger, Nigeria, Senegal, Sudan na Zambia.
Leave a Reply