DPP alivyozimwa kumshtaki wakili mshukiwa wa ulaghai wa ardhi – Taifa Leo


WAKILI anayedaiwa kuilaghai familia ya mfanyabiashara aliyefariki shamba mtaani Eastleigh jijini Nairobi, amepata afueni.

Hii ni baada ya mahakama kuu kumzuia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kumshtaki.

Ni Jaji Wendy Micheni aliyewazuia maafisa wa polisi kumkamata na kumfikisha kortini Salim Ali Mwadumbo kwa shtaka la utapeli wa ardhi ya thamani ya Sh110 milioni.

Mali hii inamilikiwa na familia ya marehemu Modhihiri Mohamed Modhihiri.

Jaji Micheni alimpa afueni ya siku 12 Bw Mwadumbo ili kupisha kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi aliyowasilisha mshukiwa katika mahakama kuu.

Jaji huyo aliamuru kesi hiyo itajwe tena Disemba 13, 2024 kwa maagizo zaidi.

Ombi la kumzima DPP na polisi wasimfungulie mashtaka Bw Mwadumbo, liliwasilishwa na wakili Wandati.

Bw Wandati alieleza mahakama kuu kwamba haki za wakili huyo zitakandamizwa iwapo mahakama haitapiga breki mpango wa kumfikisha kortini mshtakiwa ili kujibu mashtaka.

Jaji Micheni alielezwa kuwa DPP aliwasilisha hati ya mashtaka mbele ya hakimu mkuu Benmark Ekhubi mnamo Jumatatu (Disemba 4,2024) na kuamuru Mwadumbo afike kortini Disemba 5, 2024 kujibu mashtaka licha ya kuelezwa alikuwa amelezwa hospitalini.

“Endapo hii mahakama haitaingilia kati na kusitisha kushtakiwa kwa Bw Mwadumbo haki zake zitakandamizwa kwa sababu kuna kesi nyingine katika mahakama kuu kuhusu ardhi hiyo iliyoko Eastleigh,” Jaji Micheni alifahamishwa na wakili wa mshtakiwa.

Baada ya kukabidhiwa nakala ya agizo la mahakama kuu, Bw Ekhubi alisitisha  kusikizwa kwa kesi hiyo hadi Disemba 17,2024.

Jaji Micheni aliamuru Mwadumbo awakabidhi DPP, Inspekta Jenerali wa Polisi, Idara ya Uchuguzi wa Jinai (DCI) na Mwanasheria Mkuu nakala za kesi hiyo pamoja na hati za kesi.

Bw Ekhubi alielezwa kwamba mbali na agizo hilo la kuzuia kushtakiwa Mwadumbo amelazwa hospitalini na hata “asingefika kortini.”

Alhamisi wiki iliyopita, binti wa kambo wa mjane wa Modhihiri Mohamed Modhihiri alishtakiwa kwa kula njama ya kumlaghai shamba hilo la thamani ya Sh110m.

Nadra Modhihiri Mohamed alikana mashtaka ya kula njama ya ulaghai na kughushi hati za umiliki wa shamba hilo na kuandikisha shamba hilo kwa jina jingine kinyume cha sheria.

Bi Nadra alidaiwa kutekeleza uhalifu huo Novemba 5, 2011 mahali pasibainika akishirikiana na watu wengine.

Alikana shtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni na mdhamini mmoja.

Hakimu mwandamizi Bw Gilbert Shikwe alimpa dhamana badala ya bondi ya Sh300,000 pesa tasilimu.

Familia ya Modhihiri inawakilishwa na Ammar Abubakar aliyeambia mahakama kuwa mshtakiwa ameanza mikakati ya kukabili asasi husika za serikali kupinga kushtakiwa.

Mawakili Ian Mutiso (kushoto), Danstan Omari na David Mokaya wakiwa kortini. Picha|Richard Munguti



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*