Drama za jezi, watimkaji kuzimia Hong Kong Marathon Kipkemboi akiponyoka na Sh8 milioni – Taifa Leo


WAKENYA Bethwell Kipkemboi, Kennedy Kipyeko na Anderson Seroi walifagia nafasi tatu za kwanza mtawalia kwenye mbio za Standard Chartered Hong Kong Marathon zilizoshuhudia kizaazaa kilichosababisha watimkaji watatu kupoteza matokeo yao.

Kipkemboi alitwaa taji la mbio za wanaume za kilomita 42 kwa saa 2:11:13 akifuatwa kwa karibu na Kipyeko (2:11:35) na Vincent Kiprono (2:11:49).

Hata hivyo, Kiprono alipoteza nafasi ya tatu kwa bingwa wa mwaka 2024 Seroi aliyekuwa amekamata nafasi ya nne. Kiprono alikuwa mwathiriwa wa kuvalia bibu tofauti na iliyofaa kuwa yake.

Bethwell Kipkemboi  akielekea kuibuka mshindi wa mbio hizo Jumapili. PICHA | HISANI

Vincent Lam, Wong Kwun-hang na Wong Kai-lok walinufaika na masaibu ya bibu ya He Yingbing na Sun Xiaoyang katika mbio za 21km.

Yingbing na Xiaoyang walikuwa wamekamata nafasi mbili za kwanza wakifuatiwa na Lam, Kwun-hang na Kai-lok, lakini wakapoteza matokeo kutokana na tatizo hilo.

Mbali na mkanganyiko wa bibu, Hong Kong Marathon 2025 ilishuhudia angaa watimkaji sita wakikimbizwa hospitalini baada ya kuzidiwa na hali ya anga.

Mshindi wa 42km alitia mfukoni Sh8.3 milioni nao nambari mbili na tatu Sh3.8m na Sh1.9m mtawalia.

“Nafurahi. Ushindani mkali ulinitia hofu na kunifanya nijitume zaidi. Barabara za mashindano pia zilinipa changamoto, lakini nilifanikiwa kuibuka mshindi kwa sababu nilijiandaa vyema nchini Kenya,” akasema Kipkemboi aliyetawala Mersin Marathon nchini Uturuki mnamo Desemba 2024.

Nafasi tatu za kwanza kitengo cha wanawake ziliwaendea Volha Mazuronak kutoka Belarus (2:27:00) na Waethiopia Emebet Niguse (2:28:03) na Tadelech Bekele (2:28:15). Makala hayo yalivutia washiriki 74,000.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*