Enzi za machifu wenye nguvu zarudi wakipatiwa polisi – Taifa Leo


SERIKALI ya kitaifa inapanga kuajiri maafisa wa polisi kusaidia Maafisa wa Utawala wa Kitaifa hatua ambayo imesawiriwa kama juhudi za kurejesha machifu waliokuwa na nguvu kupita kiasi kabla ya katiba kubadilishwa 2010.

Kitengo kipya cha maafisa wa utawala wa kitaifa a (NGAPU), kinanuiwa kuimarisha uwezo wa serikali kutimiza majukumu yake.

Uongozi wa Polisi wa Utawala ulieleza kuwa maafisa watatumwa katika kitengo hicho mara moja, huku maafisa 19,000 wa ziada wakiajiriwa katika awamu mbili ndani ya miaka mitatu ijayo.

Maafisa 6,000 wa kwanza wataajiriwa ili kuendeleza uhusiano wa kihistoria kati ya Polisi wa Utawala na  maafisa hao wa utawala wa serikali ya kitaifa.

Ilipendekezwa kuwa kundi la awali la maafisa wa kitengo hicho, ambao bado watafuata  amri ya polisi iliyopo, wanapaswa kutoka kwa Polisi wa Utawala kabla ya wapya kuajiriwa.

Kulingana na kamati ya kiufundi iliyoanzisha NGAPU, kitengo hicho kinalenga kusaidia  maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa kuratibu shughuli za serikali ya kitaifa kote nchini.

Mnamo Agosti 20, 2024. Rais aliagiza Wizara ya Masuala ya Ndani na  Utawala wa Kitaifa, kwa ushirikiano na Inspekta Jenerali wa Polisi, kuanzisha kitengo ili kusaidia maafisa wa utawala wa serikali katika kusimamia usalama

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Polisi wa Utawala wa 2025-2028, Mwenyekiti wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi, Isaac Hassan, aliwahakikishia Wakenya kwamba maafisa hao hawatakuwa na nguvu kupita kiasi, kama ilivyokuwa mwanzoni mwa miaka ya 2000.

“Nakumbuka miaka ya 2000, Wakuu wa Mikoa walikuwa na madaraka makubwa kwa sababu walikuwa na askari polisi. Wakenya wanahofia kurudi kwa enzi hizo. Ninataka kuwahakikishia Wakenya kwamba hili halitafanyika,” alisema Hassan.

Kamishna wa Ukanda wa Nairobi Kate Mwanza alibainisha kuwa Kenya tayari inakabiliwa na uhaba wa maafisa wa polisi na akapendekeza kuwa Polisi wa Kitaifa wa Akiba kuzingatiwa wa huduma hizo.

Katibu  wa Wizara ya Usalama wa Ndani na Utawala Raymond Omolo, alieleza kuwa kitengo hicho kipya kiliunda kufuatia mapendekezo kutoka ripoti ya jopokazi  Kazi  iliyoongozwa na Jaji Mstaafu David Maraga.

“Tuna Polisi wa Utawala na NGAO wanaofanya kazi pamoja kutatua mizozo vyema,” alisema Omolo.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alisema NGAPU itaimarisha utoaji wa huduma kwa Wakenya wa kawaida.

“Serikali inajua kuwa Polisi wa Utawala ni sekta muhimu ya usalama wa nchi. Tuna historia ndefu kati ya Polisi wa Utawala na maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa. Leo, tunazindua NGAPU ili kujaza mapengo na kusaidia mashirika ya serikali kutekeleza majukumu ya serikali ya kitaifa. Hii ni pamoja na kudumisha sheria na utulivu, kutatua migogoro, na kupigana na pombe haramu,” alisema Murkomen.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*