FAMILIA moja katika kaunti ndogo ya Matungu, Kakamega ilirudisha michango iliyotolewa na wanasiasa kuisaidia kugharamia mazishi ya chifu mkuu wa zamani.
Mchango huo ulitolewa kabla ya makabiliano makali kuzuka wakati wa mazishi, jambo ambalo liliathiri hafla hiyo.
Haya yanajiri huku polisi katika eneo la Magharibi wakiwaita wanasiasa watatu kurekodi taarifa kufuatia makabiliano yaliyozuka wakati wa mazishi ya Agostino Odongo kutoka kijiji cha Chibanga wadi ya Mayoni mnamo Jumamosi.
Familia ya marehemu chifu, Bw Odongo, bado ina hasira baada ya baba yao kukosa kupokea heshima za mwisho kutokana na hali tete iliyozuka wakati mazishi yakiendelea.
Ibada ya mazishi ilikumbwa na vurugu baada ya wafuasi wa Gavana Fernandes Barasa kuzozana na wale wa aliyekuwa waziri Bw Rashid Echesa na Mbunge wa Matungu, Bw Peter Nabulindo, huku wakirushiana viti na kusababishia wengi majeraha na uharibifu wa mali.
Familia hiyo iliwashutumu Mabw Echesa na Nabulindo kwa kupanga vijana hao kuvuruga hafla ya mazishi.Mnamo Jumatatu, familia ilirudisha ng’ombe na Sh15,000 ambazo zilitolewa na Bw Nabulindo na Sh50,000 ambazo zilitolewa na Bw Echesa.
“Leo, tumerudisha ng’ombe na pesa tulizopewa kama michango ya mazishi na mbunge wa eneo letu, Bw Nabulindo. Pia tumerudisha pesa tulizopewa na Bw Echesa. Hili linafaa kuwa funzo kwa wanasiasa,” akasema Bw Patrick Luttah, mwanawe marehemu Odongo.
Alisema baba yao alikuwa mtu aliyeheshimika na hakujihusisha na siasa na mazishi yake yalistahili heshima lakini wanasiasa hao wawili walizua vurugu na kufanya mazishi hayo kutokuwa na taratibu.
Msimamo wa kijasiri wa familia hiyo umeibua mjadala kuhusu ongezeko la visa vya wanasiasa kugeuza hafla za mazishi kama eneo la vita na vurugu wakijaribu kuonyesha ubabe wao kisiasa.
“Bado nina kiwewe na kile kilichotokea. Tangu tulipomtunza baba yetu hadi kufariki kwake, ni jambo la kusikitisha sana mtu kugeuza mazishi yake kuwa eneo la kujipigia debe kisiasa. Baba yetu alizikwa haraka, hatukupata muda wa kuzungumza kuhusu baba yetu. Ni mbaya sana,” aliongeza Bw Luttah.
Alizitaka mamlaka husika kuwachukulia hatua waliohusika na vurugu hizo.Kamanda wa polisi wa eneo la Magharibi, Bw Kiprono Langat, alisema wamewaita wanasiasa hao watatu (Barasa, Nabulindo na Echesa) kufika mbele ya afisa wa upelelezi wa makosa ya jinai wa eneo hilo kuhojiwa.
Leave a Reply