CHAMA cha Wiper, kimemtimua Mbunge wa Daadab Farah Maalim kufuatia matamshi aliyohusishwa nayo ya kutusi vijana ambao wamekuwa wakiendeleza maasi dhidi ya utawala wa Rais William Ruto.
Wiki jana, Bw Maalim akiandamana na Rais William Ruto katika Kaunti ya Uasin Gishu, alitumia maneno mazito dhidi ya wanaopinga utawala wa sasa na kusema hawatafaulu.
Alhamisi, Januari 16, 2025, Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka alitangaza kuwa Bw Maalim ambaye aliwahi kuhudumu kama naibu spika wa Bunge la Kitaifa kati ya 2007-2013, amefurushwa chamani.
Pia, alipoteza wadhifa wake kama naibu kiongozi wa chama hicho cha upinzani.
“Kwa kuondoa shaka yoyote, Mheshimiwa Farah Maalim ambaye amekuwa akihudumu kama naibu kiongozi wa Wiper, ametimuliwa chamani. Amekiuka Katiba kwa kuwatusi vijana akiwataja kama wajinga na kuwatusi mama zao,” akasema Bw Musyoka.
“Alikuwa mwanamageuzi na nilimfanyia kampeni Dadaab. Inaniuma sana kuwa anaweza kutoa matusi kama hayo na kuanzia sasa ametimuliwa kutoka Wiper,” akaongeza makamu huyo wa rais wa zamani.
Uamuzi wa kumtimua Bw Maalim, 69, uliafikiwa baada ya mkutano wa baraza kuu la Wiper katika afisi za chama hicho Nairobi.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa Wiper hakuweka wazi iwapo Bw Maalim alikuwa amepewa nafasi ya kujitetea kabla ya kuangushiwa adhabu hiyo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Kisiasa, mwanachama hufurushwa iwapo amekiuka Katiba ya chama.
Kabla ya kuchukuliwa hatua hiyo, anastahili kuagizwa kufika mbele ya asasi mbalimbali za chama ili aadhibiwe japo kwa kuzingatia Katiba ya chama.
Mbunge huyo anatarajiwa kujibu Wiper kuhusu kutimuliwa kwake na hatua atakayochukua kuhakikisha kuwa hapotezi kiti chake cha ubunge kabla ya 2027.
Akiwa kwenye ziara hiyo na Rais, Bw Maalim alieleza imani yake kuwa Ruto atashinda muhula wa pili bila kutokwa jasho kutokana na jinsi ambavyo amechapa kazi hasa kwa watu wa Kaskazini mwa Mashariki.
Vilevile, alisema utendakazi wa Rais kwa muda wa miaka miwili ambayo amekuwa mamlakani, unatosha kumvunia tuzo ya hadhi ya Nobel.
“Tangu uhuru tukivuka daraja la Garissa, tulikuwa tukisema tunaenda Kenya. Sasa tuna miradi yote ya maendeleo ambayo imeanzishwa na Rais na ni mara ya kwanza tunajihisi kama Wakenya,” akasema Bw Maalim.
Mwaka jana, 2024, wakati maandamano ya Gen Z yalikuwa yameshika kasi nchini, Bw Maalim alijipata pabaya kwa kudai angepatiwa nafasi, basi angewadhuru zaidi ya vijana 5,000 ambao walikuwa wamevamia Bunge la Kitaifa.
Kauli hiyo kama tu ya juzi, ilichemsha mtandao na kusababisha vijana wengi kumshambulia wakimtaja kama kiongozi ambaye amejishusha hadhi na si kielelezo chema kwa Wakenya.
Julai 2024, NEC ya Wiper ilipendekeza Bw Maalim afurushwe chamani na kuvuliwa unaibu kiongozi wa chama lakini mbunge huyo hakutetereka.
Kauli hiyo pia ilisababisha aagizwe kufika mbele ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano Nchini (NCIC).
Leave a Reply