ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amelaani ghasia zilizozuka katika hafla iliyoandaliwa na mkewe Pasta Dorcas Rigathi mjini Jumamosi, Januari 18, 2025.
Pasta Dorcas alikuwa katika hafla ya maombi huko Nyeri iliyovamiwa na aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Maina Njenga, akiandamana na vijana wafuasi wake.
Pasta Dorcas alilazimika kuondoka ghafla kupitia mlango wa nyuma vurugu zilipozuka Bw Njenga alipofika.
Akijibu, Bw Gachagua alinyooshea serikali kidole cha lawama “kwa kumtuma” Njenga kuvuruga mkutano wa maombi. Gachagua alishutumu serikali kwa kuachilia magenge ya wahalifu ili kuvuruga mkutano wa maombi ya amani.
“Kumtuma kiongozi wa genge la wahalifu walioharamishwa na wasaidizi wake kuvuruga maombi ya amani na kuchafua madhabahu ndio hali duni kabisa ambayo Serikali inaweza kufikia,” Gachagua alisema kupitia Twitter.
Bw Njenga na wafuasi wake waliokuwa katika msafara wa magari kadhaa walipovamia uwanja huo mwishoni mwa sherehe wakiimba ‘Ndovu! Ndovu’ huku Bw Njenga akiwa juu ya paa la gari lake la Toyota Prado chini ya ulinzi mkali.
Jambo hili linaonekana kuwashangaza waandalizi wa hafla hiyo, huku mhubiri mmoja anayeishi Nairobi maarufu kama Padri Maina wa OTC akikatiza maombi yake ya mwisho na kurejea kwenye kiti chake mkanyagano ukizuka huku mamia ya waumini wakikimbilia usalama katika njia tofauti.
Hata hivyo, baada ya ibada kutatizwa kwa muda mfupi Bw Njenga alikaribishwa katika jukwaa kuu ambapo alijiunga na makasisi walioonekana kutikiswa na mabadiliko hayo. Alijiepusha na siasa licha ya wito wake wa hivi majuzi kwa wakazi wa eneo la Mlima Kenya kumuunga mkono rais William Ruto.
Leave a Reply