Gachagua alazimika kukimbilia usalama wake mazishi yakigeuka uwanja wa fujo – Taifa Leo


WAKAZI katika eneo la Limuru, Kaunti ya Kiambu, waligubikwa na mshangao na hamaki baada ya ibada ya mazishi ya bloga maarufu eneo hilo, iliyohudhuriwa na aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, kugeuka ghafla uwanja wa fujo.

Familia, jamaa na marafiki walizidishiwa majonzi huku wakilazimika kukimbilia usalama wao baada ya watu wanaodaiwa kuwa wahuni wa kulipwa, kuzua tafrani kwa kuvunjavunja viti na kung’oa hema iliyosheheni viongozi maarufu akiwemo Bw Gachagua, aliyeondolewa hapo upesi na wasaidizi wake.

Picha na video zilizosambazwa mno kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha gari lililomsafirisha Bw Gachagua kuhudhuria ibada hiyo likiwa limevunjwa vioo huku waombolezaji waliokumbwa na mshtuko wakipiga mayowe wasijue la kufanya.

Yote yalianza wakati wa kutoa hotuba katika ibada ya kumuaga buriani Bw Erastus Nduati Muigai, 23, iliyofanyika katika Shule ya Upili ya Bibirioni Boys.

Bw Muigai aliyefahamika kwa lakabu ya Mwene Limuru, alikuwa bloga maarufu wa masuala ya kisiasa katika kundi linalofahamika kama Uteti wa Limuru.

Seneta wa Kaunti ya Kiambu, Karungo wa Thangwa, Mbunge wa Kajiado Kusini Onesmus Ngogoyo, mbunge wa zamani Limuru, Peter Mwathi, aliyekuwa diwani wa Lari, John Karichu ni miongoni mwa wanasiasa walioandamana na naibu rais wa zamani kuhudhuria mazishi hayo.

Juhudi za kuwasiliana na Seneta wa Kiambu hazikufua dafu.

Katika ghasia hizo, watu kadhaa walijeruhiwa akiwemo mlinzi wa Bw Gachagua, kulingana na diwani wa zamani, aliyezungumza na Taifa Leo.

“Nipo salama lakini nimekimbia hospitalini kupeleka marafiki wangu wawili waliojeruhiwa na pia mlinzi wa Riggy G,” alisema akichelea kutajwa.

Kilichofuata ni kurushiana lawama baina ya wanasiasa huku baadhi ya wakazi wakiwashutumu wanasiasa eneo hilo akiwemo Mbunge wa Limuru John Kiragu na aliyekuwa mbunge Peter Mwathi, kwa kuvuruga mazishi.

Tukio hilo linalosemekana kumlenga Bw Gachagua, lilizuka siku chache tu baada ya naibu rais huyo wa zamani kupokonywa walinzi.

“Nilipokuwa nimeandamana na mheshimiwa Rigathi Gachagua kuhudhuria mazishi Limuru, tulishambuliwa na wahuni waliojipanga vilivyo katika mkondo wa kusikitisha sana wa matukio. Inashangaza kuwa wanaompinga Bw Hachagua sasa wamegeukia ghasia za kikatili na uhuni,” alisema Mbunge wa Mukurueni, John Kaguchia.

Mbunge huyo alihoji, “hii ndiyo sababu ulinzi wake uliondolewa? Ninataka kuwaeleza waliopania kusababisha michafuko kukoma kwa sababu hali hii inaelekeza taifa letu pabaya.”

Kulingana na mkazi eneo hilo, Joyce Mburu, kundi la vijana walilipwa Sh1,000 kila mmoja ili kuvuruga mazishi hayo.

Hata hivyo, baadhi wametilia shaka watu walioonekana kujua kuhusu mipango ya kuzua ghasia baada ya kuthibitisha kuwa Bw Gachagua angehudhuria.

Juhudi za kuwasiliana na Seneta Thangwa hazikufua dafu.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*