Gachagua atapatapa akiahirisha tena kutangaza chama cha ‘kutikisa’ Ruto 2027 – Taifa Leo


KWA mara nyingine, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumapili alikosa kutimiza ahadi yake ya kuzindua chama kipya anachohoji kitatikisa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Gachagua, alitarajiwa kuzindua chama chake mwishoni mwa Januari mwaka huu, kama alivyokuwa ameahidi baada ya masaibu ya kubanduliwa mamlakani Oktoba 2024.

Kinyume na ilivyotarajiwa na wengi kwamba angetimiza ahadi hiyo mnamo Jumapili, Februari 9, 2025 hilo halikutendeka hatua inayofasiriwa kuwaweka kwenye njia panda wafuasi wake.

Kwenye mahojiano Jumapili usiku na vituo vya runinga na redio vinavyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Agikuyu, naibu huyo wa rais wa pili wa Kenya chini ya Katiba ya 2010, badala yake alisema muungano utakaokuwa na sura ya kitaifa utazinduliwa mwezi Mei mwaka huu.

Akikilinganisha kama jengo lenye msingi thabiti na imara na gari jipya, Bw Gachagua alidai kwamba chama hicho kitakachomenyana na Rais Ruto 2027 ki tayari.

“Mwezi wa tano, ndio tutazindua gari hilo jipya, nambari yake ya usajili ili watu wajue rangi yake,” Bw Gachagua akasema.

Aidha, alihoji kwamba chama hicho kitakuwa muungano wenye sura ya kitaifa licha ya kuwa asili yake ni Mlima Kenya.

Gachagua alitangaza kuwa kitafungua matawi yake kote nchini, na kurejesha wafuasi wake waliomezwa na chama cha UDA – kinachoongozwa na Rais Ruto, Alisema analenga kuandikisha wafuasi milioni 5.5.

Bw Gachagua mnamo Jumapili akitetea sababu zake za kutofichua majina ya chama, akitumia mfano wa gari jipya, alidai anahofia lisizuiwe kuelekea kwenye kituo cha magari kuchukua abiria.

“Gari letu liko tayari, liko kwenye duka la magari mapya na sehemu zake zote ni mpya, yakiwemo magurudumu. Dereva wake, ni mtu wa zamani na anaitwa Rigathi wa Gachagua, ambaye ana tajiriba ya muda mrefu na hawezi kulitumbukiza kwenye mtaro.

“Kati ya duka na kituo cha magari, linaweza kuzuiwa kwa mawe na huyu mtu kwa sababu ninamjua. Sitafichua nambari za usajili kwa sasa. Watu wamejaa kituoni wakisubiri liwabebe,” Bw Gachagua alielezea, akitumia matamshi yaliyoonekana kumsuta Rais Ruto.

Mbunge huyo wa zamani Mathira, alisema sababu za kuunda chama kipya zinatokana na alichodai “jamii ya Mlima Kenya imesalitiwa na Dkt Ruto licha ya 2022 kumpa zaidi ya kura milioni nne”.

Bw Gachagua alisema, ameshawishiwa na jamii anayotoka na Wakenya kuunda muungano ambao utakomboa taifa.

Alijipigia debe akihoji alisaidia Ruto kuvuna kura milioni 4.4 kutoka eneo pana la Mlima Kenya, ambalo uchaguzini humezewa mate na kila mgombea urais.

Dkt Ruto alihudumu kama naibu rais kati ya 2013 na 2022, na alimenyana na kinara wa ODM aliyewania urais kupitia mrengo wa Azimio, Ruto akisaidiwa na mgombea mwenza, Rigathi Gachagua, na waliibuka washindi.

Bw Odinga aliungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta – ambaye kwa sasa amestaafu.

Ruto alizoa kura 7,176,141 (asilimia 50.49 ya kura zilizopigwa), akiafikia kigezo cha Katiba cha asilimia zaidi ya 50 na kura moja mgombea kuwa rais kwa awamu ya kwanza, dhidi ya mpinzani wake, Odinga aliyepata kura 6,942,930 (asilimia 48.85).

Bw Gachagua, kwenye hafla za umma amekuwa akisisitiza kwamba ndiye alimsaidia Rais Ruto kuzoa kura za ushindi kufuatia ushawishi wake Mlimani.

Kutokana na kubanduliwa wadhifa wa naibu rais 2024, Gachagua Jumapili alirejelea kauli ngome yake ilighadhabishwa na hatua hiyo “na ndiposa Ruto anapokea upinzani mkuu eneo la Kati.”

Alikiri kufanya kosa 2022 kuingia mkataba na Ruto bila chama, akisema sababu zinazomfanya Bw Odinga kila baada ya uchaguzi licha ya kutoibuka kidedea, huchumbiwa na serikali kwa ajili ya kuwa na chama imara – ODM.

“Sisi kama ‘nyumba’, tulijiunga na UDA tukijua kuwa ni chama kizuri na kitatupeleka mbele. Sisi tumemalizana na UDA, na hatutarejea humo tena,” Bw Gachagua alisema, akisisitiza kuwa maamuzi ya kubuni chama yanatokana na shinikizo la jamii kutoka Mlima Kenya.

Aliongeza, “Nyumba yetu inasema tulifanya kosa kubwa sana; tulienda harusi na gari la wenyewe. Tulijiunga na chama cha Ruto ilhali yeye ndiye mwenye cheti cha umiliki wa gari na dereva, na tulipofika kwenye mto akatuamuru tushuke tuende harusini miguu, akachukua watu wengine.”

Hata ingawa hatua ya Gachagua kuchelea kuzindua chama kunakanganya wafuasi wake na kubashiriwa kuwa karate ya siasa, alisema tayari jamii ya Ukambani – aliyohoji sasa ni Mlima Kenya Kusini, Maasai, Kisii na eneo la Magharibi mwa Kenya, zimeahidi kuwa kwenye muungano wake na kwamba zimejinyakulia nafasi chamani.

“Kati ya sasa na Mei, tunalenga jamii ya Mijikenda, Kuria na Kalenjin, na maeneo mengine ya nchi yapate nafasi za uongozi chamani.”

Gachagua pia alisema vijana wa Gen Z, aliotuhumiwa kuchochea kuandamana dhidi ya serikali ya Ruto 2024 watakuwa na usemi mkubwa kwenye chama atakachozindua.

Akiamini kitamfanya Ruto kuingia kwenye kumbukumbu za rais wa kwanza kuhudumu muhula mmoja Kenya, alisema analenga kiwe na zaidi ya wabunge 100, maseneta 17 na madiwani (MCA) wasiopungua 700, ili kiwe na usemi bunge la kitaifa, seneti na mabunge ya kaunti.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*