Gachagua hapumui shida zikimuandama tangu madaraka yaishe – Taifa Leo


TANGU kuondolewa afisini, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amekuwa akiandamwa na mikosi, mikutano yake ikigubikwa na ghasia huku naye akilaumu serikali kwa kumakinika kumkata miguu ya kisiasa.

Baada ya kungátuliwa mnamo Oktoba 18, 2024 na juhudi zake za kusalia afisini kugonga mwamba, mikutano yake imekuwa ikikumbwa na ghasia huku wandani wake nao wakidai kuandamwa na makachero kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI).

Hapo jana Jumamosi, Desemba 28, 2024, Bw Gachagua alilengwa kwa vitoaa machozi wakati ambapo alihudhuria ibada ya makanisa mbalimbali katika bustani ya Shamata, Kaunti ya Nyandarua.

Gesi hiyo ya kutoa machozi ilirushwa na mwanaume ambaye alikuwa amevalia nguo za raia, ilimlenga Bw Gachagua japo ilizuiwa na mmoja wa walinzi wake kabla kumfikia.

Walinzi wa Bw Gachagua kisha walimzingira na kumpeleka kwenye gari lake la kibinafsi ambalo lilikuwa umbali wa mita 10 kutoka mahali ambapo alikuwa ameketi.

Umati ulimvamia mwanaume aliyerusha gesi hiyo ya kutoa machozi wakampiga na kumjeruhi vibaya lakini akaokolewa na maafisa wa polisi.

Umma ulimwandama mwanaume huyo hata baada ya polisi kumwokoa na ikawalazimu maafisa hao wa usalama watumie gesi za kutoa machozi na kufyatua risasi hewani kuwatawanya.

Raia waliwakashifu polisi wakidai walikuwa na ajenda fiche na walikuwa wakilenga kumdhuru Bw Gachagua ndiposa walimwokoa mwanaume huyo.

Mnamo Novemba 28, Bw Gachagua alilazimika kuchana mbuga na kutoroka katika mazishi moja Limuru baada ya ghasia kuzuka na wahuni kuwavamia waombolezaji.

Mitandaoni alichapisha habari kuwa serikali ilikuwa imempokonya walinzi ili kufaulisha uvamizi huo ambao ulitokea kwenye mazishi ya Erastus Nduati.

Mnamo Disemba 19, Bw Gachagua alidai kuwa afisa wa DCI alikuwa amemfuata hadi wadi ya Kalawa, eneobunge la Mbooni Kaunti ya Makueni.

Alikuwa amesafiri umbali wa kilomita 200 kudhuria mazishi katika eneobunge hilo. Bw Gachagua alishauri serikali impe afisa huyo kazi ya kuwalinda Wakenya badala ya kutumia mafuta kumfuatilia.

Aidha wandani wake hasa wabunge, wamekuwa wakidai kuhangaishwa na DCI huku akisema kuwa hatatereka na ataendelea na juhudi zake za kuunganisha Mlima Kenya.

Tukio la kurushwa kwa vitoza machozi jana lilitokea baada ya Seneta wa Nyandarua John Methu kumaliza kuwahutubia raia na alikuwa karibu kuwaalika wengine wahutubu.

Baada ya ghasia hizo, raia walisema wameafikiana kuwa polisi hawafai kutoa ulinzi katika mikutano ya Bw Gachagua wakiahidi kuwa watamlinda wenyewe.

Maafikiano hayo yaliungwa mkono na viongozi wa kisiasa ambao walikuwa katika hafla hiyo. Mnamo Ijumaa jioni, waandalizi wa mkutano huo walikuwa wameshutumu serikali kwa kupanga kuuvuruga.

Walimlaumu Mbunge Mwakilishi wa Kike Faith Gitau na Mbunge wa eneo hilo George Gachagua wote ambao walikuwa wamepiga kura kuhakikisha kiongozi hiyo anabanduliwa kutoka wadhifa wake wa unaibu rais.

Akihutubu, Bw Gachagua alimlaumu Rais William Ruto kutokana na ghasia hizo akisema wale ambao wapo serikalini wanastahili kumakinika kutoa huduma kwa Wakenya badala ya kumlenga kisiasa.

“Rais anastahili kufahamu kwa nini Wakenya wana hasira na hawezi kuwalazimisha wampende. Tukio hili linaonyesha uoga na hawezi kuendelea kuwaumiza Wakenya kwa kuonyesha maoni yao katika mikutano ya umma,” akasema Bw Gachagua.

“Tulikuwa na Moi ambaye alikuwa dikteta na alienda nyumbani. Mbinu hizo zimepitwa na wakati na hazitafanya kazi katika enzi ya kisasa,” akaongeza.

Seneta Methu naye alisema Rais Ruto alikuwa amejaribu kuzima mkutano huo.

“Tunamwaambia rais kuwa unaweza kukataa kujenga barabara na kutunyima miradi lakini huwezi kutuzuia kukutana na kuandaa maombi,

“Lazima uheshimu makanisa na viongozi wa kidini wala hatutaingiwa na uoga na kutii amri yako ya kututishia kwa kutumia maafisa wa usalama,” akasema Seneta Methu.

“Hapa Mlima Kenya Gachagua ndiye kiongozi wetu na unastahili kuelewa hilo. Tutaendelea kumpenda na kuhudhuria mikutano yake,” akaongeza.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*