Gachagua na Karua wazika tofauti zao, waponda Ruto – Taifa Leo


ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua jana alizika tofauti zake za kisiasa na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na wakatangaza kuwa watashirikiana kulipa eneo la Mlima Kenya mwelekeo kisiasa.

Bw Gachagua, mkewe Dorcas na washirika wake, walimtembelea Bi Karua nyumbani kwake Gichugu Kaunti ya Kirinyaga ambapo walimshambulia Rais William Ruto na serikali yake kwa utawala mbaya.

Mkutano huo, ambao ulijaa hisia za kisiasa, ulijiri kukiwa na minong’ono kuhusu juhudi za kuleta umoja wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.

Bw Gachagua alisema amezika tofauti zake na Bi Karua na kuanzia sasa watakuwa wakishauriana katika safari ya kukomboa Kenya kutoka utawala wa Kenya Kwanza.

“Nimefika hapa kukutana na kushauriana na dadangu Bi Karua ambaye ni kiongozi jasiri anayependa kutetea haki. Hata wakati wa kampeni tulipokuwa pande tofauti katika mashindano ya kisiasa katika uchaguzi mkuu, nilikuwa nikitamani ungekuwa upande wetu,” alisema Bi Gachagua.

Katika uchaguzi huo, Gachagua alikuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto katika muungano wa Kenya Kwanza naye Bi Karua akiwa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika muungano wa Azimio.

Bw Gachagua alipuuza madai ya Rais Ruto kwamba anaendeleza siasa za ukabila ilhali alimuunga mkono Dkt Ruto licha ya kuwa anatoka kabila tofauti.

Akihutubia wakazi wa Kaunti ya Busia mnamo Januari 23, 2025, Rais Ruto aliashiria kuwa Gachagua aliondolewa mamlakani kwa kuendeleza siasa za ukabila na ufisadi na kumtaka akome kukosoa serikali kutoka “vichakani” kwa kuwa alishindwa na kazi.

Bw Gachagua alisema matamshi ya Rais yanatokana na uchungu wa kuachwa na eneo la Mlima Kenya kwa kuwa alilisaliti licha ya kumpigia kura kwa wingi katika uchaguzi wa 2022.

“Mimi, Rigathi Gachagua, si mkabila kwa sababu nilimuunga mkono Rais William Ruto ilhali yeye si wa jamii yangu. Asilimia 87 ya watu wa jamii yangu walimpigia kura, wakijua vyema kwamba yeye si wa jamii yao,” Gachagua alisema.

“Sisi ni wazalendo, na ni dharau kwa jamii hii kwa rais kuzunguka akituita wakabila. Tunajua kwamba hana furaha, amechanganyikiwa, na ana uchungu kwamba watu wetu wamemuacha.

”Gachagua alikuwa akimjibu Ruto kuhusu matamshi aliyoyatoa huko Vihiga siku ya Jumatano, ambapo alimkosoa Naibu Rais huyo wa zamani kwa kutokuwa na uwezo, ukabila, na fisadi.

 

“Kuna watu wanaojaribu kutuingiza katika siasa za chuki na za kikabila ambazo zina nia ya kuwagawanya Wakenya. Kuna watu tuliowapa kazi, lakini kwa sababu hawana akili na ni wafisadi, walizama na wataendelea kuzama,” Ruto alisema.

Bi Karua pia alimkemea Rais Ruto, akimshutumu kwa udikteta na ukiukaji wa Katiba hasa kutokana na visa vya utekaji nyara.

“Unapopewa nafasi ya uongozi, tambua haumiliki Kenya, Kenya si mali yako- ni yetu sote. Huwezi kuanza kufanya mambo ambayo hayapo kwenye Katiba. Tutasema ‘hapana’ kwa sababu mamlaka ni ya raia,” Karua alisema.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*