Hadhihakiwi Rabana – Taifa Leo


Ni kwa nguvu za Kahari, mumba mbingu na dunia ,
Amilikiye bahari, waja na wanyama pia,
Natunga hili shairi, nikupe wangu usia,
Hadhihakiwi Rabana, hasira zake hudhuru.

Aliishi tangu dahari, na ndivyo atasalia,
Haitaji daktari, wala ndwele kumjia,
Maandiko yanakiri, hana mtani Jalia,
Hadhihakiwi Rabana, hasira zake hudhuru.

Ajigotaye kidari, sifa kujimiminia,
Akamtweza Kahari, hishima kumvunjia,
Humkumba tahayuri, na mwisho hujililia,
Hadhihakiwi Rabana, hasira zake hudhuru.

Zimesambaa habari, Amerika inalia,
Imewagubika nari, jijini Califonia,
Kwa kufanya ujeuri, wengi wameangamia,
Hadhihakiwi Rabana, hasira zake hudhuru.

Mijengo ya kifahari, ilokuwa yavutia,
Na ya gharama magari, majivu yamesalia,
Kila pembe ni hatari, mji wameukimbia,
Hadhihakiwi Rabana, hasira zake hudhuru.

Mola ametema mori, na funzo kuwapatia,
Wamepokwa utajiri, wote walo’jivunia,
Kimewashuka kiburi, hawana cha kuringia,
Hadhihakiwi Rabana, hasira zake hudhuru.

Si mageni yano’jiri, vitabu vyasimulia,
Tangu enzi za Asheri, pamoya na Anania,
Nabii walibashiri, na ndiyo yanatukia,
Hadhihakiwi Rabana, hasira zake hudhuru.

Hapa nasema kwaheri, tamati nimefikia,
Nimekumegea siri, neno langu zingatia,
Sijifanye jemadari, akachukizwa Jalia,
Hadhihakiwi Rabana, hasira zake hudhuru.
FRANK ORINA,
JOMVU MADAFUNI MOMBASA

Muda na nafasi
Kushukuru hakudhuru, shukurani kwake Mola,
Kufaana hakudhuru, tusioneane ila,
Kuwafanya wakufuru, wakashindwa wao kula,
Muda na nafasi zipo, itika nikuitapo.

Itika nikuitapo, nirekebishe narai,
N’eleze papo hapo, palipo na uhai,
Nikihitaji uwepo, uwepo nikiauni,
Muda na nafasi zipo, undugu ni kufaana.

Undugu ni kufaana, sio kule kufanana,
Tufaane kuzikana, pia kuelekezana,
Narai ‘sikonyoana, chanzo chetu kutengana,
Muda na nafasi zipo, ‘situtawale zahama.

‘Situtawale zahama, tukaingia Sodoma,
Kwenye giza tukazama, maisha yakatulema,
Tukasalia kuhema, tukaya’cha yalo mema,
Muda na nafasi zipo, nitie moyo na nguvu.

Nitie moyo na nguvu, wanipigano kalamu,
Niepusha na maovu, nionyeshe yalo tamu,
Nikanye kuwa mvivu, niwe mwenye umuhimu,
Muda na nafasi zipo, bila zetu samahani.
Bila zetu samahani, tuishi kama zamani,
Simwone na walakini, ukamtia motoni,
Yasome yake matini, utajifunza yakini,
Muda na nafasi zipo, tuishi kama zamani.
ABRAHAM KIPLANG’AT
RAUSI FALSAFA
CHUO KIKUU CHA LAIKIPIA

Jitu lisiloulika

Ni lini litaulika? , langu swali nauliza,
Nani ana uhakika, aweze kutueleza,
Mioyo yaungulika, nani atatuangaza,
Jitu lisiloulika, Wakenya limetuchosha.

Ni tangu zama za zama, likuwepo jitu hili,
Wageni lipotukoma, yalisalia makali,
Latufanyia unyama, na kuzidi tudhalili,
Jitu lisiloulika, Walimu limetuchosha.

Tutumie gani njia, jitu tuje langamiza,
Wasomi mutatwambia, lisidizi tuumiza,
Watafiti nanyi pia, wanguwangu mtujuza,
Jitu lisiloulika, Wakulima metuchosha.

Mbona sasa viongozi, hawatilii manani?
Wametilia ajizi, wakenya twaumiani,
Ama sio yao kazi, jitu hili jitu gani?
Jitu lisiloulika, wazalendo metuchosha.

Hata wapi ukienda, jitu hili talikuta,
Misuli yake meeunda, lakututia ukata,
Ni kipi tuweze tenda, tutowe wake utata?
Jitu lisiloulika, Watabibu metuchosha.

Kaditama ninafika, langu swali ninafunga,
Nambeni kwa uhakika, niweze upata mwanga,
Nimechoka kusumbuka, kuhusu hili janga,
Jitu lisiloulika, Washairi metuchosha.
VINCENT OKWETSO
“MALENGA OKWETSO”
MAGHARIBI MWA KENYA

Mke wa bosi
Naomba hiyo kalamu, nifanye nikipendacho,
Ninayo mambo muhimu, yanayoniwasha macho,
Mke wa bosi karimu, ana mambo kochokocho,
Mke wa bosi jamani, nakusihi uniache.

Yapata mwaka mmoja, nikifanya kazi kwake,
Bwana wake ni meneja, kampuni za kakake,
Mkewe hunipa luja, kwa nyingi hisia zake,
Mke wa bosi jamani, sitaki kwenda kinyume.

Navyonidekeza mja, kufanya kazi kagoma,
Mapenzi yake lahaja, isojua taaluma,
Ananonyesha vioja, mawazo yanisakama,
Mke wa bosi jamani, wewe ni rika ya mama.

Ng’ombe hazeeki ini, kila siku anasema,
Akilivaa gauni, husema ‘simwite mama,
Anasema hadharani, namlemaza mtima,
Mke wa bosi jamani, siwezi kufanya hilo.

Ye huniita chumbani, ndani kwake kitandani,
Anaanza kwa utani, kuniweka miguuni,
Namwambia siwezani, kuzamia kilindini,
Mke wa bosi jamani, mfanyikazi watesa.

Mdalasini napewa, mapochopocho macheo,
Nguo zote nafuliwa, cha mumewe hicho cheo,

chakula napakuliwa, kila siku kitoweo,
Mke wa bosi jamani, nakusihi uniache.

EZEKIEL NZEKE (KARMA)
MIKOBA YA BABU
MBUINZAU

Tuache chuki
Tupendane washairi, kwa nini tuchukiane?
Na tuombeane heri, siku zote tufunzane.
Ni gumu hii safari, yahitaji tushikane,
Tupendane ndugu zangu,sichukie ndugu yako

Kwa nini uwachukie, ndugu zetu washairi?
Kwa nini siwachukue, uwafunze ushairi?
Wivu usikuzidie, ukajiona hodari,
Tupendane ndugu zangu,sichukie ndugu yako

Mlo juu ulingoni, naomba wacheni chuki,
Walo chini wapendeni, wafanyeni marafiki,
Vyema waelekezeni, waondoleeni dhiki,
Wote mnaoandika, daima wacheni chuki.

Tunajenga nyumba moja, ni ya nini sasa chuki
Heri tuwe na umoja, kisha tuwe marafiki,
Kuchukia wetu waja, hilo kwetu sio haki,
Tupendane ndugu zangu, tukome kuchukiana.

Naomba niambieni, chuki hufaidi nini?
Si vizuri kwenye fani, nawaomba tuacheni,
Mwisho wetu kaburini, sasa chuki ni ya nini?
Waandishi tuna chuki, na twajenga nyumba moja.

Hata mkinichukia, ukweli nitausema,
Wacheni kulia ngoa, nawaomba wanadama,
Leo nimewaambia, jambo hili linauma,
Tupendane ndugu zangu, daima tuache chuki.
DENNIS NGATIA
CHUO KIKUU CHA KARATINA

Matokeo yametoka
Matokeo keshatoka, yale ya watahiniwa,
Wengine walishituka, wakati walipojuwa,
Wengi walilalamika, wengine washangiliwa,
Matokeo keshatoka, hivyo basi mujipange.

Usiwe nayo wahaka, ni mpango wa Moliwa,
Wewe dada wewe kaka, ni vyema kujitambuwa,
Matokeo yakitoka, ni heri kujielewa,
Matokeo keshatoka, hivyo basi mujipange.

Usije kubabaika, kwa kozi kuichaguwa,
Sasa umeelimika, na kwa sasa mwajijuwa,
Mbali nayo mutafika, mkiweka pia duwa,

Matokeo keshatoka, hivyo basi mujipange.

Msije kutatizika, ni mengi mumeambiwa,
Mfahamu kwa hakika, kozi nzuri kuchaguwa,
Msiwe nayo haraka, kwa kuweza kuamuwa,
Matokeo keshatoka, hivyo basi mujipange.

Kalamu chini naweka, hapa sasa ninatuwa,
Msiwe nayo haraka, popote hata mkiwa,
Mambo yatabadilika, hata mutafanikiwa,
Matokeo keshatoka, hivyo basi mujipange.
MALENGA KITONGOJINI,
LIONEL ASENA VIDONYI.
TONGAREN, NDALU

Japo mefeli mtihani
Matokeo yalitoka, ila yanihuzunisha,
Mwenzenu nimeanguka, mwenzenu sina bashasha,
Kabisa nimekereka, alama zahuzunisha,
Nimefeli mtihani, lakini sio maisha.

Niliitia bidii, tatizo sijafahamu,
Waalimu nilitii, na bado mambo magumu,
Nikahaidi jamii, ‘takavyoipa elimu,
Nimefeli mtihani, lakini sio maisha

Wazazi siwalaumu, kweli waliwajibika,
Likawa langu jukumu, kufanya nililotaka,
Lakini kwenye kalamu, kweli nimeaibika,
Nimefeli mtihani, lakini sio maisha.

Jamii ninakuomba, usije kunifokea,
Maisha sio sambamba, kila siku twaponea,
Na kisima ukichimba, lazima maji kunywea,
Nimefeli mtihani, lakini sio maisha.

Naomba radhi walimu, wasomi ni tofauti,
Na hapa najifahamu, kufeli sio mauti,
Nikalifanya jukumu, akili ‘kanisaliti,
Nimefeli mtihani, lakini sio maisha.

Beti sita nakomea, tena nina ujasiri,
Mlopita nawombea, kama ilivyo desturi,
Mwenzenu sitachelea, natafuta mshauri,
Nimefeli mtihani, lakini sio maisha.
EZEKIEL J NZEKE (KARMA)
CHUO KIKUU CHA MURANG’A (CHAKIMUT)

 

Jukwaa la mahaba
Nasimama jukwaani, kumtaja wangu hani,
Ni mrembo si kiwani, katu simwonei soni,
Kumtaja hadharani, huyu wangu wa ubani,
Jina lake tambueni, kwamba anaitwa Wini.

Ni mwenye njema tabia, uzuri wakuvutia,
Rangi yake asilia, dukani hajanunua,
Mwenye sauti murua, hata kiwa analia,
Sichoki kumsifia, mjukuu wa Kizua.

Nahisi hakusumbua, shule alipo somea,
Masomo kuzingatia, hapo alitia nia,
Hesabu nayo kemia, zote alizibukua,
Nami ninajivunia, mke aliyetulia.

Pongezi nawapatia, wazazi walomlea,
Daima naiombea, ile yao familia,
Izidi kumpa njia, ya mema kuyaendea,
Apate kuyatumia, kwenye yetu familia.
 DEO D. TITUS
SINGIDA TANZANIA

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*