MASWALI yameibuka iwapo Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka atadumu katika jangwa la kisiasa linalomkodolea macho kwa kutengwa na vigogo wa siasa za kitaifa waliokuwa naye katika upinzani.
Huku Bw Musyoka akikaa ngumu katika upinzani, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta aliokuwa nao katika muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja One Kenya wamemchangamkia Rais William Ruto na serikali yake ya Kenya Kwanza.
Tayari, Bw Odinga ameongoza chama chake cha ODM kujiunga na serikali na tetesi zinaashiria kuwa handisheki ya Dkt Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenya itafanya viongozi wa chama cha Jubilee waliokuwa wakimuunga Bw Musyoka kuteuliwa serikalini.
Duru zinasema Bw Musyoka amekataa kumchangamkia Dkt Ruto licha ya kiongozi wa nchi kumkaribisha kwa mikono miwili.
Baada ya Bw Odinga kuridhiana na Dkt Ruto na ODM kujumuishwa katika serikali, Bw Musyoka alijitangaza kuwa kiongozi rasmi wa upinzani mwaminifu kwa watu na tangu wakati huo amekuwa akikosoa serikali.
Iwapo ukuruba mpya wa Dkt Ruto na Uhuru utapelekea wandani wa rais huyo wa nne kujiunga na serikali, Bw Musyoka huenda atabaki na kiongozi wa DAP- Kenya Bw Eugene Wamalwa upande wake pekee miongoni mwa vinara wakuu wenza wa Azimio.
Wachambuzi wa siasa wanasema inasubiriwa kuona iwapo Bw Musyoka ambaye alionekana kuungwa mkono na viongozi wa muungano wa jamii za Mlima Kenya, Gema, atadumu kivyake katika mawimbi ya siasa za Kenya.
“Bw Musyoka anaonekana kuwa katika jangwa la kisiasa kwa wakati huu baada ya kukataa kuchangamkia Dkt Ruto kama vinara wenzake wa Azimio isipokuwa Martha Karua ambaye aliondoa chama chake katika muungano huo wa upinzani na Eugene Wamalwa ambaye wamekuwa wakitembea pamoja hadi sasa,” asema mchanganuzi wa siasa Jairus Okemwa.
Anaongeza: “ Japo sio wa kupuuzwa katika siasa za Kenya ikizingatiwa ana ngome inayochukua mwelekeo mmoja wa kisiasa ilivyofanya katika uchaguzi wa 2017 na 2022, anaonekana kutengwa na vigogo wa kisiasa za kitaifa huku akisisitiza atagombea urais,” asema.
Ikizingatiwa inategemea muungano wa kisiasa kushinda urais, kutengwa kwa Bw Musyoka kunamuweka katika hali hatari.
“Hali ikidumu ilivyo hadi 2027, azima ya Bw Musyoka inaweza kutibuka. Lakini iwapo anaweza kuvutia Wakenya ambao wamekerwa na sera za serikali ambayo wenzake katika upinzani wanachangamkia, na iwapo Mlima Kenya hautarejesha imani kwa Ruto, anaweza kutoka katika jangwa la kisiasa, iwe kupitia ushirika mpya kabla au baada ya uchaguzi,” asema Okemwa.
Bw Musyoka ndiye kiongozi wa pekee wa Azimio aliyekosoa hotuba ya Rais Ruto Siku ya Jamhuri, akimshutumu kiongozi wa nchi kwa kuota.
Katika taarifa kupitia anwani yake ya X, Musyoka alitaja hotuba hiyo kama ya kujipongeza iliyopambwa kwa ukweli feki kupotosha umma.
Kiongozi huyo wa Wiper alishutumu utawala wa Kenya Kwanza kwa kusaliti itikadi za mashujaa wa uhuru wa Kenya, ambao alisema walipigana kishujaa kukomboa taifa kutoka kwa ukandamizaji wa wakoloni.
‘Hayo si maono ya watangulizi wetu, ambao walijitolea kutukomboa kutoka kwa nira ya ukoloni,’ Kalonzo alisema.
Kiongozi wa Chama cha Wiper alitoa wito wa umoja na upinzani dhidi ya kile alichokitaja kuwa utawala wa kikatili.
Seneta wa Makueni Bw Dan Maanzo amenukuliwa akisema kwamba ‘mnamo 2027 Bw Musyoka ataungana na vyama vingine ambavyo havijumuishi Rais Ruto’.
Alisema ‘tayari tunachangamkia ambao wamekasirishwa na utawala mbovu unaodhihirika kote, kutojali hisia za Wakenya na tabia ya kutokubali ukweli’.
Kufikia sasa, Bw Musyoka anaonekana kuwania Mlima Kenya kuelekea 2027.
Aidha, kuna minong’ono kwamb anawalenga Bw George Natembeya na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Ndani Dkt Fred Matiang’i miongoni mwa wengine.
Leave a Reply