BAADA ya kujikusanyia jumla ya pointi nne kwenye mechi mbili zilizopita, kikosi cha Harambee Stars kinahitaji tu sare kufuzu kwa fainali ya mashindano ya Mapinduzi Cup nchini Zanzibar.
Wenyeji Zanzibar wanatarajiwa kuwa wapinzani wakuu wa Harambee Stars, lakini sare ya aina yoyote ama ushindi utakiwezesha kikosi hicho cha kocha Francis Kimanzi kufuzu kwa fainali itakayofanyika Januari 13.
Timu hiyo inayojumuisha wanasoka wanaosakatia klabu za hapa nchini ilianza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Burkina Faso kabla ya kubwaga Tanzania 2-0, mabao yaliyofungwa na Boniface Muchiri na Ryam Ogam.
Wakenya wamekuwa wakilalamika kuhusu uchezaji wa Harambee Stars wakidai hauna mpango, lakini wengi waliofuatilia mechi hizo mbili wameanza kushuhudia tofauti kubwa ikilinganishwa na kikosi cha Engin Firat.
“Tulianza mechi hizo kwa kuzuia kushindwa na lengo letu ni kutwaa ubingwa,” Kimanzi alisema kuhusu mashindano hayo ambayo mshindi ataondoka na Sh6.25 milioni, timu itakayomaliza katika nafasi ya pili ikipokea Sh4.35 milioni ilhali Sh3.1 milioni zitatolewa kwa timu itakayomaliza katika nafasi ya tatu.
Harambee Stars haijakuwa katika hali nzuri hasa chini ya kocha Firat aliyetimuliwa baada ya timu hiyo kushindwa kufuzu kwa fainali za 2025 AFCON zitakazofanyika nchini Morocco.
Hata hivyo, kikosi cha Kimanzi na wasaidizi wake, Zedekiah Otieno na John Kamau kimeanza kuwasisimua Wakenya.
Kwenye mchujo wa kufuzu kwa AFCON, Harambee Stars ilimaliza katika nafasi ya tatu katika Kundi J kwa pointi sita, Indomitable Lions ya Cameroon ikiibuka mshindi wa kundi hilo.
Zimbabwe ilimaliza ya pili na kufuzu, huku Namibia ikimaliza ya mwisho kwa pointi mbili.
Makinda Muchiri, Ogam, Daniel Sakari, James Kinyanjui, Kelly Madada, Brian Musa, Michael Mutinda, Siraj Mohammed na Darius Msagah ni miongoni mwa wachezaji wanaovumisha kikosi cha Kimanzi.
Katika Mapinduzi Cup, Harambee Stars na Burkina Faso kila moja inajivunia pointi nne, lakini Stars wako mbele kutokana na ubora wa mabao. Zanzibar wana pointi tatu ilhali Tanzania wako mkiani bila chochote.
Leave a Reply