HATUA ya Rais wa Amerika Donald Trump ya kusitisha shughuli za Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Amerika (USAID) kunatishia sekta ya kilimo nchini Kenya wiki chache kabla ya msimu muhimu wa upanzi, na hivyo kuathiri mamilioni ya wakulima kote nchini wanaotegemea mipango mbalimbali inayofadhiliwa na nchi hiyo.
Wakulima wa Kenya wanatayarisha mashamba yao kwa msimu wa mvua na hatua ya Trump itazima mipango ya thamani ya mabilioni katika kaunti 27, ambapo USAID imekuwa msingi wa maendeleo ya kilimo.
Katika Kaunti ya Makueni, kwa mfano, ambapo asilimia 47 ya familia zinakabiliwa na uhaba wa chakula, USAID ilikuwa imezindua mradi kabambe wa Mifumo ya Chakula nchini unaotarajiwa kutekelezwa hadi 2029.
‘Mradi huu ulikusudiwa kuleta mabadiliko kwa wakulima wetu,’ afisa mmoja kutoka kaunti hiyo alisema.
Mpango huo, unaotekelezwa na TechnoServe, ulilenga kushughulikia lishe, ustahimilivu wa wakulima, na faida kwa wafanyabiashara wadogo.
Athari za kusitishwa kwa shughuli za USAID zitaonekana kwa njia tofauti katika maeneo mbalimbali yanayotegemea kilimo nchini Kenya. Katika eneo la Magharibi, linalojumuisha kaunti kama Bungoma, Busia, na Kakamega, mpango wa USAID wa Feed the Future umekuwa muhimu katika kuleta mapinduzi ya kilimo.
Kaunti ya Bungoma, kwa mfano, imefaidika kwa kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuboresha upatikanaji wa soko, na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
‘Tumeona maendeleo ya ajabu katika mifumo yetu ya thamani ya maziwa na mahindi,’ afisa mmoja wa kaunti hiyo alisema.
‘Kusimamishwa kwa ghafla kwa mipango hii kunaweza kurudisha nyuma mafanikio ya miaka mingi katika mabadiliko ya kilimo,” aliongeza.
Katika eneo la Mashariki, kaunti zikiwemo Meru, Tharaka Nithi, Machakos, Makueni, Kitui, na Taita Taveta zimekuwa zikipokea usaidizi maalum kulingana na changamoto zao mahususi za kilimo.
Mradi wa Kenya Agricultural Value Chain Enterprises (KAVES) umekuwa ukifanya kazi hasa katika maeneo haya, ukilenga kubuni mifumo muhimu ya thamani katika sekta za maziwa, mahindi na kilimo cha bustani.
Hatua ya kusitisha USAID inatishia mipango kadhaa muhimu ambayo imekuwa uti wa mgongo wa maendeleo ya kilimo nchini Kenya.
Mradi wa Mfumo wa Soko la Mazao na Maziwa nchini (KCDMS), ambao unafanya kazi katika kaunti nyingi, umekuwa muhimu katika kuimarisha mifumo ya soko katika sekta ya kilimo cha bustani na maziwa. Vilevile, mradi wa Kuimarisha Uvumbuzi wa Maji ya Kilimo (STAWI) umekuwa muhimu katika kuboresha usimamizi wa maji kwa kilimo, hasa katika maeneo yenye ukame.
Usaidizi wa kifedha wa USAID umekuwa muhimu vile vile.
Katika mwaka wa 2018 pekee, mpango wa Feed the Future ulifadhili wafanyabiashara na wakulima wadogo 42,000, kuwezesha kwa mikopo ya takriban Sh567.6 milioni na kuchangia Sh132 milioni katika uwekezaji mpya wa sekta ya kibinafsi.
Jumla ya msaada wa USAID kwa kilimo nchini Kenya inakadiriwa kuwa wa mabilioni ya pesa.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply