Hawa ni Manchester United! Kinda Amad Diallo awazika Man City kwao Etihad – Taifa Leo


MANCHESTER United waliduwaza Manchester City 2-1 kupitia mabao ya dakika za lala salama katika vita vya vilema kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), uwanjani Etihad, Jumapili.

Red Devils wa United waliingia mechi hiyo wakiwa wamepoteza mara tatu mfululizo ligini ugani Etihad. Walinusia rekodi yao ya kupoteza mechi nne mfululizo za EPL nyumbani kwa City waliyoweka kati ya mwaka 1952 na 1955, wakati City waliongoza kwa muda mrefu 1-0.

Difenda wa Man City, Josko Gvardiol (kushoto), asherehekea na Ruben Dias baada ya kufungua ukurasa wa mabao uwanjani Etihad. PICHA | REUTERS

Katika mechi hiyo City walikuwa wakifukuzia ushindi wa pili katika mechi 11 katika mashindano yote msimu huu, mabingwa hao watetezi waliongoza kwa dakika 87 baada ya kupata goli dakika ya 36 kutoka kwa Josko Gvardiol.

Raia wa Croatia, Gvardiol sasa ndiye beki amefunga mabao mengi kuliko beki mwingine yeyote kwenye ligi hiyo ya klabu 20 tangu msimu 2023-2024. Gvardiol ana mabao manane.

Msimu huu pekee, Gvardiol amefungia City mabao manne. Alifunga bao la hivi punde kupitia kichwa kutokana na krosi ya kungo mbunifu Kevin De Bruyne iliyoguswa na mshambulizi wa United, Amad Diallo.

Hata hivyo, United ya kocha Ruben Amorim, ambayo ilikuwa imepoteza dhidi ya Arsenal 2-0 (Desemba 4) na Nottingham Forest 3-2 (Desemba 7), ilisawazisha kupitia penalti ya nahodha Bruno Fernandes dakika ya 88 kabla ya Diallo kufunga bao la ushindi dakika mbili baadaye.

Amad Diallo baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya City. PICHA | REUTERS

City ya kocha Pep Guardiola, ambayo sasa imepoteza dhidi ya United mara tatu mfululizo 2-1 katika mechi tatu zilizopita kwenye mashindano, sasa inasalia na alama 27 kutokana na mechi 16 katika nafasi ya nne, nyuma ya nambari tatu Arsenal kwa pointi tatu.

Liverpool ya kocha Arne Slot inaongoza kwa alama 36 baada ya kujibwaga uwanjani mara 15 ikifuatiwa na Chelsea.

Vijana wa Amorim wanapatikana katika nafasi ya 12 kwa alama 22 baada ya kuruka Tottenham Hotspur ambao wana mechi moja mkononi.

Bao hilo la Diallo (pili kushoto) la ushindi lilisababisha sherehe katika kikosi kizima cha Manchester United. PICHA | REUTERS

Katika mchuano mwingine uliosakatwa Jumapili, wageni Crystal Palace walifunga mabao yote wakilemea Brighton 3-1 ugani Amex.

Palace waliongoza 3-0 kupitia mabao ya Ismaila Sarr (mawili) na Trevor Chalobah kabla ya Marc Guehi kupatia Brighton la kujifariji baada ya kujifunga dakika ya 87.

Ni mara ya kwanza Palace walishinda Brighton kwa zaidi ya goli moja tangu Desemba 2012 walipowapiga 3-0 katika Ligi ya Daraja la Pili.

Imeandaliwa na GEOFFREY ANENE



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*