MAGEUZI ya kisiasa yanaendelea kushika kasi nchini huku wanasiasa wakionekana kuungana kwa lengo la kumtuma Rais William Ruto nyumbani mnamo 2027.
Kwa sasa makundi mbalimbali ya kisiasa yameanza kujisuka kwa ajili ya uchaguzi wa 2027, huku vigogo wakilenga kuhakikisha kuwa Rais Ruto anajipata pabaya kihistoria kwa kuhudumu muhula moja pekee.
Mnamo Jumamosi, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua aliridhiana na Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua licha ya kuwa walikuwa na uhasama mkali kati uchaguzi wa mnamo 2022.
Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i amejitokeza kuwa mpinzani mkali wa Rais Ruto kwenye kura ijayo huku akiungwa mkono na baadhi ya viongozi wa jamii ya Abagusii. Pia kuna fununu kuwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta yupo nyuma ya Dkt Matiang’i baada ya Katibu wa Jubilee Jeremiah Kioni kusema chama hicho kinaunga azma yake.
Rais Ruto haonekani kupumua ambapo Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka naye amekuwa akimkashifu usiku na mchana kuhusu uongozi wa taifa. Bw Musyoka ambaye tayari ana eneo la Ukambani nyuma yake, analenga kuwa debeni mnamo 2027 baada ya kulemewa kwenye kura za 2007.
Aidha makundi ya Gen Z ambayo yamekuwa yakishiriki vita vikali dhidi ya Rais Ruto mitandaoni, pia yanadaiwa kuweka mikakati ya kumuunga mkono mmoja wao ili kuingia ikulu.
Hatua ya Bi Karua na Bw Gachagua kuridhiana inaonekana kama mbinu ya kuhakikisha kuwa Rais Ruto anapoteza kura za Mlima Kenya ambazo zilichangia asilimia 47 za kura zote alizopata mnamo 2022.
Rais Ruto anaonekana ana kibarua cha kurejesha eneo hilo nyuma yake baada ya Bw Gachagua kutimuliwa madarakani mnamo Oktoba mwaka jana. Uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki unaonekana haujaridhisha eneo hilo huku wanasiasa wanaounga mkono utawala wa sasa wakiendelea kukabiliwa vikali na raia.
Mnamo Machi, 2024, tofauti za Bi Karua na Bw Gachagua zilishamiri kuelekea Kongamano la Limuru III ambapo aliyekuwa naibu rais alipinga sana hafla hiyo akisema lililenga kuondoa Mlima Kenya serikalini.
Wakati huo, Bw Gachagua alisema ndiye alikuwa kiongozi mwenye wadhifa mkubwa serikalini kutoka eneo hilo na iwapo kulikuwa na suala lolote basi Bi Karua na Katibu wa Jubilee Jeremiah Kioni, wangeshauriana naye.
Kuzika tofauti zao kwenye wikendi kunaonyesha ari ya Mlima Kenya kuelekeza kura zao kwenye debe moja 2027. Aidha Bw Gachagua anatarajiwa kuzindua chama kipya mwezi ujao, hali ambayo huenda ikadhoofisha zaidi umaarufu wa UDA Mlima Kenya.
“Mlima Kenya wana uwezo wa kihela, idadi ya watu lakini hawana mtu anayevutia maeneo mengine ya nchi. Sasa hivi hawana viongozi wenye utaifa kama marehemu Kenneth Matiba na Mwai Kibaki na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta,” akasema Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Javas Bigambo.
“Gachagua mambo yake yote Mlima Kenya ni kumpiga vita Rais Ruto na ukimwondoa Rais nguvu zake za kisiasa zitaisha. Karua naye si kivutio na huenda analenga ugavana na kutamba siasa za nyumbani ndiposa amekumbatia maridhiano hayo,” akaongeza.
Bw Matiang’i naye anafuata nyayo za marehemu Simeon Nyachae ambaye aliwania urais mnamo 2002 na kuibuka wa tatu. Tayari Seneta wa Kisii Richard Onyonka na Bw Kioni wamesema watamuunga mkono mnamo 2027.
“Tumeamua kuwa tutamuunga Dkt Fred Matiang’i kama mgombeaji wetu wa urais katika uchaguzi mkuu ujao. Atawania urais kwa tiketi ya chama ambacho kitasukwa kwenye msingi wa haki, uwazi na maadili, ajenda yake kuu ikiwa ni utoaji huduma,” akasema Bw Onyonka.
Tangazo la Bw Onyonka lilijiri baada siku chache baada ya Dkt Matiang’i kukutana na wabunge 10 kutoka kaunti za Kisii na Nyamira kama sehemu ya mikakati yake ya kusaka uungwaji kutoka eneo hilo anakotoka kabla ya kupanua mawanda yake maeneo mengine ya nchi.
Bw Musyoka, 71 naye ameweka wazi kuwa mara hii lazima awe debeni na anaendelea kujisuka kisiasa kupitia muungano wa Azimio, akionekana kupata uungwaji mkono wa Kiongozi wa DAP Eugene Wamalwa.
Bw Musyoka ashatalikiana kisiasa na Kinara wa Upinzani Raila Odinga japo anaonekana pia siasa zake za kushutumu ODM kujiunga na serikali, zimekuwa zikiungwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.
Kiongozi huyo amekuwa akijisawiri kama sauti ya upinzani huku wandani wake wa kisiasa wakisema 2027 ni wakati muafaka wake kuingia ikulu.
Shinikizo hizi zitamlazimu Rais Ruto kucheza kadi ya juu kisiasa hasa wakati huu ambapo amehakikishiwa uungwaji mkono wa ODM.
Leave a Reply