VIONGOZI wa kibiashara wanaweza kusaidia kuunda sera zinazokuza ukuaji wa uchumi wa muda mrefu na uendelevu nchini Kenya iwapo wataingia bungeni.
Mjasiriamali Kevin Otiende, alisisitiza jukumu muhimu la biashara katika uchumi wa Kenya, akibainisha kuwa sekta hiyo inaajiri zaidi ya asilimia 95 ya wafanyakazi.
Hata hivyo, alidokeza kuwa wafanyabiashara hawajawakilishwa vilivyo katika Bunge, ambapo sera muhimu za kiuchumi zinaundwa.
“Biashara ni uti wa mgongo wa uchumi wetu, na tunahitaji viongozi katika Bunge ambao wanaelewa utata, changamoto na uwezo wake,” alisema Otiende.
Aliongeza: “Kuwa na viongozi kama hao katika bunge kutahakikisha maamuzi ambayo yanalinda masilahi yetu ya kiuchumi na uendelevu wa biashara wa muda mrefu.”
Bw Otiende pia alisisitiza umuhimu wa kuwachagua wabunge wanaotetea sera zinazokuza uvumbuzi na kusaidia katika ustawi wa wafanyikazi, hasa kwa kuzingatia tatizo la kuachishwa kazi linaloathiri sekta nyingi.
Data kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu Kenya (KNBS) inaonyesha uwezo wa sekta ya kibinafsi katika kushughulikia ukosefu wa ajira.
Utafiti wa Uchumi wa 2024 ulibaini kuwa viwanda kama vile kilimo, misitu, uvuvi na biashara za rejareja vilichangia zaidi ya asilimia 16 ya ajira katika sekta binafsi mwaka 2023.
Biashara Ndogo na za Kati (SMEs), ambazo zinawakilisha zaidi ya asimilia 90 ya sekta ya kibinafsi, huajiri. zaidi ya Wakenya 14.9 milioni.
Biashara hizi sio tu muhimu kwa maisha bali pia ni kichocheo kikuu cha ukuaji wa Pato la Taifa la Kenya, kupunguza umaskini na maendeleo ya uchumi.
“Ili kutambua uwezo kamili wa sekta ya kibinafsi Kenya, tunahitaji mazingira ya kisera thabiti na yanayoweza kutabirika. Hili linaweza tu kuafikiwa ikiwa watu wengi zaidi wenye nia ya biashara watachaguliwa kuwa Wabunge ili kupitisha sheria zinazosaidia ukuaji endelevu,” asema Otiende.
Otiende anaamini utaalam wa wafanyabiashara unaweza kutekeleza jukumu muhimu katika kuunda sera zinazofungua uwezo wa kiuchumi wa nchi, kuunda nafasi za kazi, na kuendeleza maendeleo endelevu.
“Sekta ya kibinafsi ni nguvu ya uwezo, lakini inahitaji wawakilishi katika Bunge ambao wanaelewa mahitaji na fursa. Kwa sera zinazofaa, tunaweza kubadilisha uchumi wa Kenya na kuboresha maisha ya mamilioni ya watu,” Otiende aliongeza.
Leave a Reply