Hivi yani viti ni silaha mazishini na wakodishaji wanahitaji kuviwekea bima! – Taifa Leo


VITI, viwe vya plastiki au mbao, vinapaswa kutambuliwa kisheria kama silaha hatari wakati wa msiba.

Nazo kampuni za kukodisha viti zinapaswa kupewa leseni maalum za kutumia silaha hizo hatari kujitafutia kipato.

Vilevile, tunapaswa kuwa na kampuni mahsusi za bima ya viti ili watu wakiumizwa kwavyo walipwe fidia badala ya kwenda nyumbani kuuguza majeraha kwa chumvi na maji ya vuguvugu.

Nao waombolezaji wanaotumia viti kupigana wanapaswa kuadhibiwa, sawa na anavyofanyiwa yeyote anayetumia silaha kumuumiza mwenzake katika mazingira tofauti.

Wewe cheka tu, na ukitaka useme hizo zitakuwa sheria duni, lakini fahamu kwamba unaposoma makala hii, haikosi kuna mtu anayekandwa mbavu kwa tambara la zamani lililochanika likakosa kazi nyingine.

Kosa lake pekee ni kwamba juzi amehudhuria sherehe za mazishi akarejea kwao na majeraha na hana bima ya SHA, SHE, SHI, SHO au SHU, wala hela au kuku mweusi wa kupeleka kwa mganga. Hata kurogesha hawezi!

Mtu ambaye ametokea mazishini akitarajia kumsindikiza marehemu kwa amani, anywe chai, ale mlo wa sherehe ya mwisho kisha arejee kwake salama anapaswa kulindwa.

Tunahitaji watu kama hao ambao wanashiriki sherehe ndogo-ndogo vijijini bila kumsumbua yeyote. Ni watu muhimu kuliko wanasiasa ambao hufika kwenye msiba kututumuliana misuli na kuonyesha mafedha.

Wanasiasa watundu wana mazoea ya kuzichapa kwa viti, ngumi na mateke hata kabla ya familia ya marehemu kutoa heshima zao za mwisho.

Kisa cha hivi majuzi zaidi kimetokea Kakamega wakati wa mazishi ya Chifu Mkuu Mstaafu Agostino Odongo. Labda wangekufanya hivyo katika msiba wa mamake Papa wa Roma, ila wakanywea kwa kujua nguvu za dola zilizokuwepo zingewasaga kama unga wa mahindi.

Nazungumzia viongozi wa kitaifa si wajumbe wa kamati za Nyumba Kumi wala wadaku wanaonong’onezeana vijijini kuhusu vijana waliotimu umri wa kuingia utu-uzima ila wanaogopa kisu cha ngariba.

Katika kisa cha Chifu Odongo, wafuasi wa Gavana wa Kakamega, Fernandes Barasa, walichaniana magwanda na wale wa aliyekuwa waziri, Rashid Echesa, na Mbunge wa Matungu, Peter Nabulindo.

Haikosi waliwajeruhi waombolezaji wengi ambao hawajui siasa. Hiyo ni dhulma kwa watu wasio na hatia. Ni maudhi tele unaposhikilia sahani la wali na nyama, kisha ghafla unasikia mshindo mkuu, kufumba na kufumbua unapata shati au rinda lako bora limemwagiliwa wali ule na mchuzi wake!

Huli ulichopakuliwa, nguo zimechafuka na labda umejeruhiwa. Anayekutendea haya anapaswa kujutia utundu wake, asiwahi kuthubutu kurudia kosa.

Washindi katika kisa cha Chifu Odongo ni wanasiasa kwa kuwa walionyesha ubabe waliokusudia, kisha wakarejeshewa michango yao ya msiba. Heri majeruhi wangetafutwa wapewe pesa hizo. Siku nyingine niulizwe tuzifanyie nini.

[email protected]



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*