WAKENYA wanapaswa kujiandaa kwa maandamano ya nchi nzima yaliyopangwa kuanza leo kulalamikia visa vingi vya utekaji nyara.
Wanaharakati wanaoandaa maandamano hayo ya nchi nzima jana walithibitisha kuwa mipango ya kuandaa ‘mama wa maandamano yote’ imekamilika.Maandamano hayo yanajiri baada ya makataa ya saa 48, yaliyotolewa Ijumaa iliyopita na wanaharakati na familia za watu wanaoshukiwa kutekwa nyara na maafisa wa usalama wa serikali, kukamilika.
Wanaharakati walikuwa wameitaka serikali kuwaachilia bila masharti watu wote wanaozuiliwa baada ya kutekwa nyara la sivyo “wapeleke malalamishi yao barabarani”.
Taifa Leo imefahamu kuwa mkutano wa siku nzima ulifanyika Nairobi jana ili kukamilisha maandalizi ya maandamano hayo yatakayofanyika katika maeneo kadhaa ya nchi huku mmoja wa wanaharakati katika mkutano huo akisema ‘kila kitu kiko tayari’.
‘Tutaandamana bila hofu hadi waliotekwa nyara waachiliwe. Hatujali itachukua muda gani. Wakati wa kuzungumza umekwisha,” alisema.
Walipokuwa wakitoa wito wa maandamano hayo wiki iliyopita, watetezi wa haki za binadamu walitaja wasiwasi mkubwa kuhusu ukatili unaofanywa na serikali.
matakwa yao
Miongoni mwa matakwa yao ni Rais William Ruto kueleza nchi ni nani hasa anayewateka nyara Wakenya huku polisi na Wizara ya Masuala ya Ndani ikikanusha kuhusika kwa vyovyote vile katika visa vya utekaji nyara wa hivi majuzi.
Walimshutumu kiongozi wa nchi kwa kufumbia macho utekaji nyara unaotokea nchini wakisema kimya chake kuhusu suala hilo kinamsaliti.Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, ambaye sasa ni mkosoaji mkuu wa Rais Ruto, pia amejiunga na wanaolaani serikali kwa utekaji nyara.
Akiwahutubia wanahabari eneo la Magharibi jana, Bw Gachagua, pamoja na viongozi wakuu wa upinzani akiwemo Kiongozi wa DAP-Kenya, Eugene Wamalwa na aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala, walitoa makataa ya saa 72 kwa utawala wa Rais Ruto kuwaachilia watu walioripotiwa kutoweka.Iwapo serikali haitatii wito huu, viongozi hao waliapa kuita Wakenya kwa maandamano kote nchini kuanzia Januari 1, 2025.
Kikosi cha siri
Siku tatu tu zilizopita, Bw Gachagua alisema kuwa kuna kikosi cha siri cha utekaji nyara, chenye makao yake katika orofa ya 21 ya jengo moja katikati mwa Jiji la Nairobi. Naibu rais huyo wa zamani aliahidi kutoa maelezo zaidi kuhusu kikosi hicho wiki hii huku akiikosoa serikali kwa kupanga utekaji nyara wa vijana kinyume cha sheria.
“Kuwateka nyara watoto hawa si suluhu. Huu ni utawala wa kwanza katika historia ya nchi hii kulenga watoto kwa ukandamizaji,” alisema.
Kufikia sasa, rekodi za Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu Kenya zinaonyesha kuna visa 82 vya utekaji nyara vilivyorekodiwa tangu Juni, 29 kati yao wakiwa hawajapatikana. Saba kati ya visa hivi viliripotiwa katika wiki mbili zilizopita pekee.
Juni mwaka huu, maandamano ya vijana wa Gen-Z yalifanyika kupinga utawala mbaya na mapendekezo ya nyongeza ya ushuru katika Mswada wa Fedha wa 2024, na kusababisha vifo vya takriban watu 61 kwa mujibu wa muungano wa mashirika kadhaa ya haki za binadamu ikiwemo Amnesty International.
Kufikia sasa, hakuna afisa hata mmoja wa polisi aliyekamatwa kwa mauaji ya kiholela, utekaji nyara au utumiaji nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano hayo, jambo ambalo limewakasirisha Wakenya wengi wanaotaka hatua ichukuliwe.
ongezeko lasikitisha
Mwenyekiti wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA), Issack Hassan alitoa taarifa kwa vyombo vya habari wiki iliyopita akisema mamlaka hiyo ‘inasikitishwa na ongezeko la visa vya utekaji nyara wa watu mbalimbali unaodaiwa kutekelezwa na polisi”.
Bw Hassan alitoa wito wa kukomeshwa kwa hali hii ya wasiwasi na akawaambia Wakenya kwamba maafisa wote watakaopatikana na hatia wanafaa kufikishwa mahakamani.
Mnamo Ijumaa, maandamano yalizuka mjini Embu ambako mmoja wa vijana saba alitekwa akisubiri kunyolewa.Maafisa wa usalama Kaunti ya Embu wametoa wito kwa wakazi kusitisha maandamano wakipinga kutekwa nyara kwa mwanafunzi wa chuo kikuu Billy Munyiri Mwangi akiwa ndani ya kinyozi.
Wakiongozwa na kamanda wa polisi wa kaunti hiyo, Bw Samuel Muthamia, maafisa hao walisema wakazi hao walikuwa wakivuruga amani na wanapaswa kuacha kujihusisha na shughuli zisizo halali.
Wakizungumza na wanahabari mjini Embu, walisema wanafanya kazi usiku na mchana kujua aliko mwanafunzi huyo na kuwataka wakazi kuwa na subira. “Tumekuwa tukimtafuta Mwangi tangu alipotoweka na wakazi wanafaa kutupa muda wa kumtafuta,” akasema Bw Muthamia.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply