KUNA hatari ya miradi ya maendeleo kukwama katika kaunti kadhaa za Bonde la Ufa baada ya mvutano kati ya madiwani na mawaziri kuibuka tena.
Madiwani wanadai kuwa baadhi ya mawaziri ni watepetevu na wabadhirifu wa rasilimali za miradi ya maendeleo.
Miongoni mwa kaunti ambazo mizozo inatokota ni Trans Nzoia na Nandi ambapo madiwani wameweka kazi za mawaziri watano hatarini kwa kuwatimua ama kuwasukuma kujiuzulu.
Gavana wa Trans Nzoia, Bw George Natembeya, ameshinikizwa kuwapiga kalamu Katibu wa Kaunti Truphosa Amere, Janerose Mutama (Waziri wa Ardhi) na Stanley Kirui (Michezo) baada ya madiwani kuunga mkono hoja ya kuwatimua.
Waliwatimua licha ya amri ya mahakama kuzuia Bunge la Kaunti kuendelea na mjadala wa kuwafurusha baada ya mawaziri kukimbilia kinga ya Mahakama Kuu ya Kitale. Mawaziri hawa walikabiliwa na tuhuma za utumizi mbaya wa ofisi, utepetevu kazini, ukiukaji wa sheria, ubadhirifu wa pesa na kumpotosha Gavana Natembeya kuhusu utoaji wa huduma za afya.
“Bw Kirui alikiuka Katiba kwa kufungua akaunti ambayo haikuidhinishwa na kuitumia kupokea mapato yaliyotumika vibaya kwa manufaa ya kibinafsi,” akasema Diwani wa Saboti, Bw Boniface Cheloti.
Katika Kaunti ya Nandi, Gavana Stephen Sang, aliinua mikono baada ya kushinikzwa afanye mabadiliko katika baraza la mawaziri. Gavana Sang alimteua naibu wake, Yulita Mitei, kuwa Kaimu Waziri wa Afya.
“Tunachotaka ni kuvunjwa kwa baraza lote la mawaziri kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao,” alisema Bw John Too, mkazi wa Kata ya Saos.
Kamati ya wanacham a15 iliyoongozwa na Bw Benjamin Kering Matata ilipendekeza kupigwa kalamu kwa mawaziri tisa na maafisa wakuu tisa miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi za juu katika idara muhimu za Kaunti ya Nandi.
IMETAFSIRIWA NA LAABAN SHABAN
Leave a Reply