KUNA hatari ya miradi ya maendeleo kukwama katika kaunti kadhaa za bonde la ufa baada ya mvutano kati ya madiwani na mawaziri kuibuka tena.
Madiwani wanadai kuwa baadhi ya mawaziri ni watepetevu na wabadhirifu wa rasilimali za miradi ya maendeleo.
Miongoni mwa kaunti ambapo mzozo unatokota ni Trans Nzoia na Nandi ambapo wawakilishi wadi wameweka kazi za mawaziri watano hatarini kwa kuwatimua ama kujiuzulu.
Katika Kaunti ya Trans Nzoia, Gavana George Natembeya ameshinikizwa kuwapiga kalamu Katibu wa Kaunti Truphosa Amere, Janerose Mutama (Waziri wa Ardhi) na Stanley Kirui (Michezo) baada ya madiwani kuunga mkono hoja ya kuwatimua.
Waliwatimua licha ya amri ya mahakama kuzuia bunge la kaunti kuendelea na mjadala wa kuwafurusha baada ya mawaziri kukimbilia kinga ya Mahakama Kuu ya Kitale.
Mawaziri hawa walikabiliwa na tuhuma za utumizi mbaya wa ofisi, utepetevu kazini, ukiukaji wa sheria, ubadhirifu wa pesa na kumpotosha Gavana Natembeya kuhusu utoaji wa huduma za afya.
“Bw Kirui alikiuka Katiba kwa kufungua akaunti ambayo haikupitishwa na kuitumia kupokea mapato yaliyotumika vibaya kwa manufaa ya kibinafsi,” akasema Diwani wa Saboti Boniface Cheloti.
Katika Kaunti ya Nandi, Gavana Stephen Sang aliinua mikono juu baada ya kushinikzwa afanye mabadiliko katika baraza la mawaziri.
Haya yalijiri baada ya wawakilishi wadi wawili – Ruth Koech (Afya) na Drice Rono (Barabara) kujiuzulu kufuatia ukaguzi wa fedha na miradi ya maendeleo ya kaunti.
Ibidi wabwage zana za kazi baada ya kamati ya ukaguzi ya miundomsingi na fedha kupendekeza kufutwa kazi kwa mawaziri na maafisa wakuu wa idara muhimu.
Gavana Sang alimteua naibu wake, Yulita Mitei, kuwa Kaimu Waziri wa Afya.
“Tunachotaka ni kuvunjwa kwa baraza lote la mawaziri kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao,” alisema John Too, mkazi wa Kata ya Saos.
Kamati ya wanachama kumi na watano iliyoongozwa na Benjamin Kering Matata ilipendekeza kupigwa kalamu kwa mawaziri tisa na Maafisa Wakuu tisa miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi za juu katika idara muhimu za kaunti ya Nandi.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan
Leave a Reply