Hofu serikali ikipunguza bima ya kibinafsi kwa watumishi wa umma – Taifa Leo


WATUMISHI wa umma wenye magonjwa sugu na kampuni za bima za kibinafsi huenda zikakabiliwa na wakati mgumu baada ya serikali kupunguza mgao kutokana na kukumbatiwa kwa Bima mpya ya Afya ya Jamii (SHA).

Serikali imekuwa ikielekeza Sh43.7 bilioni kugharimia bima ya kimatibabu ya watumishi wa umma, walimu, polisi na maafisa wa magereza. Hata hivyo, kiasi hicho sasa kimepunguzwa hadi Sh22 bilioni.Maelezo hayo yamefichuliwa kutokana na barua ya Waziri wa Fedha John Mbadi kwa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki (sasa naibu rais).

Prof Kindiki alikuwa ameomba Sh8.3 bilioni zaidi ili kugharimia bima ya matibabu kwa polisi na maafisa wa magereza.Kando na Mamlaka ya Huduma za Polisi (NPS) na ile ya Magereza (KPS), wizara, idara na asasi mbalimbali za serikali ikiwemo Tume ya Kuwaajiri Walimu Nchini (TSC) huwa zinatumia kampuni za kibinafsi kuwapa watumishi wa umma huduma za kimatibabu.

Bw Mbadi alisema pesa zinazoelekezwa kwa kampuni za bima zimepunguzwa kutokana na upungufu ambao upo kwenye bajeti ya 2024/25. Waziri huyo ameyashauri mashirika ya serikali yaangazie upya mikataba yao na kampuni za bima na iwapo patakosekana maelewano, basi wafute kandarasi hizo.

“Baraza la mawaziri lilipunguza bima inayoelekezwa kwa utumishi wa umma kwa asilimia 50 ikisubiri uhamisho hadi SHA,” akaandika Bw Mbadi kwenye barua iliyoelekezwa kwa wizara ya Usalama wa Ndani mnamo Septemba 4, 2024.

“Mnamo Agosti 30, 2024 idara ya huduma za kimatibabu ilishauri kuwa kampuni za kibinafsi za bima zitakuwa zikitoa huduma tofauti na SHA na zile ambazo hazipatikani kwa SHA,” akasema Bw Mbadi.

SHA ilianza kutumika mnamo Oktoba 1 na waziri huyo alizishauri NPS na KPS ziangazie upya mikataba yao au iikatize. Alisema mashirika yote ya serikali lazima yaoanishe mahitaji yao ili yaoane na bajeti ya 2024/25.

Aidha waziri huyo alisema kuwa kuidhinishwa kwa matumizi ya ziada kisha pesa zielekezwe kwa kampuni za bima za kibinafsi kutasambaratisha nia ya serikali ya kuhamia kikamilifu kwa SHA.

Hapo jana, Katibu wa Muungano wa Walimu Wakuu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET), Bw Akello Misori, alipinga mpango huo na kusema watatoa uamuzi wa mwisho mnamo Ijumaa wakati wa mkutano wao wa mwisho wa mwaka katika Kaunti ya Vihiga.

“Bajeti yetu haistahili kuguswa. Kabla ya 2015 wakati ambapo mpango wetu wa bima ulianza, walimu walikuwa wakilipwa marupurupu ya matibabu,” Bw Misori akaambia Taifa Leo.

Naye Katibu wa Muungano wa Watumishi wa Umma, Bw Tom Odege alisema kupunguzwa kwa mgao wa bima kutawaongezea tu Wakenya mizigo ilhali tayari wamelemewa na ushuru.

“Serikali ingeandaa mikutano ya ushirikishaji wa umma kabla ya kuchukua hatua hiyo. Watumishi wa umma tayari wamelemewa na ushuru na itakuwa vigumu kwao kuhimili mabadiliko hayo,” akasema Bw Odege ambaye pia ni mbunge wa Nyatike.

Imetafsiriwa na CECIL ODONGO

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*