Hofu wanawake 15 wakiuawa kikatili ndani ya wiki tatu! – Taifa Leo


ILIANZA kama mkasa, kisha ikawa mazoea. Hulka hiyo inaonekana kuendelea na kuwa hatari.

Kenya inakabiliana na ongezeko kubwa la mauaji yanayolenga wanawake.

Katika siku 22 za kwanza za mwaka huu pekee, angalau wanawake 15 wameuawa, katika kile kinachoonekana kuwa kuendelea kwa mtindo ulioanza karibu miaka 10 iliyopita.

Mauaji ya mwanafunzi wa darasa la saba wa miaka 14 huko Garissa Ijumaa iliyopita ni dalili kwamba hata watoto wadogo hawako salama katika nchi hii.

Mshukiwa wa mauaji ya Marianne Kilonzi, 43, ambaye alipatikana amekufa kwa kupigwa na kifaa butu nyumbani kwake London pia Ijuma wiki jana, ni dalili kwamba mauaji ya wanawake hayaheshimu mipaka ya kitaifa wala hadhi ya kijamii.

Beth Muthoni (41), Ashley Wairimu (13), Precious Nderema (13), Jane Wanjiru (26), Lydia Tokesi (29), Nancy Bonke (23), Winnie Akusuha (30), Loureen Omondi (20) na Aisha Abubakar (48) ni baadhi ya waathiriwa ambao mauaji yao yameripotiwa katika kipindi cha wiki tatu pekee zilizopita.

Miongoni mwa vifo vya hivi punde kutokana na wimbi linaloendelea la mauaji ya kinyama, ni cha Joy Fridah Munani, ambaye mauaji yake ya kutisha yaliwaacha polisi na wakazi wa mtaa wa Huruma na mshangao.

Mumewe John Kiama Wambua, 29, ambaye alifikishwa mahakamani jana jijini Nairobi, alidaiwa kukamatwa karibu na Kelly Towers akiwa ameweka kwenye begi sehemu za mwili wake zilizokatwa katwa.

Polisi walisema alikuwa akitoroka eneo la mauaji-nyumba yao mtaani Huruma.

“Wambua, ambaye alionekana kutokerwa na kugunduliwa kwa vipande vya mwili wa mkewe, aliwaongoza maafisa hadi nyumbani kwake ambapo viungo vingine vya mwili vilipatikana chini ya kitanda chake,” Idara ya Upelelezi wa Jinai ilisema.

“Katika chumba hicho damu ilijaa kwenye sakafu na hakuna tukio linaloweza kuwa la kutisha zaidi kama hilo, maafisa pia walipata kisu chenye ncha kali na nguo za mwathiriwa zikiwa zimelowa damu,” taarifa ya DCI iliongeza.

Kati ya Januari na Novemba, 2024 kulikuwa na visa 172 vya mauaji ya wanawake vilivyoripotiwa.

Hii ilikuwa ni wanawake 22 zaidi waliopoteza maisha kutoka mwaka uliotangulia, ambapo takriban mauaji 150 ya wanawake yaliripotiwa.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilionyesha kuwa kwa wastani, wanawake 47 wanauawa nchini Kenya kila wiki, wengi wao wakiuawa na watu wanaowafahamu.

Wapenzi, watu wa karibu wa familia na marafiki—watu wanaojulikana sana na wahasiriwa— wamekuwa wakigeuka wahalifu au kushukiwa katika visa vingi vya mauaji ya wanawake vinavyoripotiwa.

Mfumo wa kisheria umefanya majaribio ya kuzuia uhalifu huu wa kijinsia huku maajaji wakiwahukumu wanaopatikana na hatia kufungwa miaka mingi gerezani.

Na bado, idadi ya mauaji inaendelea kuongezeka.Baadhi ya washukiwa wako huru, na katika baadhi ya matukio hakuna washukiwa wanaokamatwa hata kidogo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*