Hotuba ya Trump ina mafunzo ya kutuzindua katika usingizi – Taifa Leo


ILIKUWA hotuba iliyojaa mbwembwe lakini ikakosa ulimbwende na ufasaha unaohusishwa na hotuba za aina hii.

Waliomtangulia katika ikulu ya White House walikuwa katika hadhira hiyo ya ufunguzi.

Hali kadhalika, walikuwepo marais na viongozi wa mataifa ya kigeni na wandani wake wenye kushabihiana naye kiitikadi.

Mikota wa teknolojia- Elon Musk, Jeff Bezos na Mark Zuckerberg walikaa safu ya mbele kabisa karibu na rais huyu na familia yake.

Katika hotuba yake, Don Trump alisistiza kwamba wakati wa kurejesha Marekani katika umaarufu wake duniani ni sasa.

Awamu yake ya pili ya urais ilidhamiria kuipa Marekani kipaumbele pamoja na raia wake.

Alilenga kufufua uchumi kwa kuboresha biashara na utozaji wa ushuru kwa namna ya kuleta tija badala ya madhila, kuimarisha usalama kwa kuilinda mipaka ya nchi na kupambana na uhalifu na ujambazi, kuboresha elimu hususan inayohubiri uzalendo na mapenzi kwa Umarekani kinyume na kuutia doa kila wakati.

Aidha, aliahidi kupambana na changamoto sugu ya uhamaji kwa kuilinda nchi kutokana na wimbi la wahamaji wa kiuchumi wanaokamia kuwa wenzi katika ndoto ya Amerika.

Pia alitia dole lake katika sega la nyuki la maadili alipoutangazia ulimwengu kwamba, Marekani ilitambua jinsia mbili tu-ume na uke.

Hotuba ya Trump imeibua hisia mseto. Kuna wale wanaomuona kama mhifadhina na mbaguzi anayeendeleza nadharia na itikadi za ugozi ambazo ziliatikwa na utumwa uliowadhalilisha sana watu wa asili ya Afrika.

Hivyo, awamu yake ya pili itazirudisha nyuma akrabu za wakati. Mkabala huu unashikiliwa na kuhubiriwa na majukwaa ya kimataifa yaliyo na hofu ya wahamaji wasiohalali kufurushwa au kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kuna wale wanaomuona Trump kama rais wa Marekani ambaye sharti ayaweke mbele maslahi ya Wamarekani. Hawa ndio waliompigia kura.

Kinachodhihirika hapa ni kwamba kiongozi ana wajibu mkubwa kwa raia wake kwanza.

Ni sharti ajitahidi kuyakidhi matakwa yao la sivyo atakijua kilichomtoa kanga manyoa.

Pili, ujasiri wa kuzungumzia waziwazi changamoto zinazokumba raia hata kama ni shubiri kwa walio pembeni huweza kumpa kiongozi umaarufu. Kenya inalandana sana na Marekani upande wa changamoto.

Uchumi unadorora, mipaka yake inavuja mno kiasi kwamba maelfu ya wahamaji wanajipenyeza nchini kwa urahisi.

Tatizo la ukimbizi lingali donda ndugu. Hii inatokana na nchi jirani kugubikwa na mizozo na vita.

Changamoto hii inaathiri usalama wa nchi. Wapika majungu ya uhasama na baadhi ya magenge ya ujambazi ni rahisi sana kupata maficho hapa nchini ikiwa vikosi vyetu vya usalama vitasinzia.

Silaha kama vile bunduki zinapatikana kwa urahisi sana na hivyo zinaweza kutumiwa kutekelezea uhalifu.

Kenya imekuwa jirani mwema kiasi cha kumshughulikia zaidi mgeni kuliko mwenyeji na mara nyingi imejipata ikilipwa fadhila zake kwa mateke ya punda.

Wakati umewadia wa uongozi wa nchi hii kujitoa bayana na kulinda mipaka yake.

Jackton Nyonje ni Meneja wa Mafunzo wa tume ya IEBC.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*