
KUSHINDWA kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) kumeendeleza kile wengi wanachokichukulia kuwa mikosi yake ya kupoteza katika uchaguzi.
Wachanganuzi wanasema hakuna muungano ambao Raila amepeperusha bendera yake ambao umewahi kushinda katika uchaguzi wa urais licha ya kuwa na ufuasi mkubwa, uzoefu na marafiki wengi wa humu nchini na kimataifa.Raila ajitosa katika uchaguzi wa urais kwa mara ya kwanza mwaka wa 1997 ambao ulikuwa wa pili chini ya mfumo wa vyama vingi vya kisiasa akiwa na chama cha NDP.
Daniel Moi wa chama cha Kanu aliibuka mshindi akifuatwa na Ken Matiba wa chama cha Ford na Mwai Kibaki wa chama cha Democratic Party akiwa wa tatu. Raila aliibuka wa nne.Katika uchaguzi wa 2002, Raila aliungana na vigogo wengine wa upinzani katika uliokuwa muungano wa Narc na wakashinda Kibaki akipeperusha bendera dhidi ya Uhuru Kenyatta wa Kanu.
Ilikuwa mara ya kwanza Kanu kushindwa baada ya kuwa mamlakani kwa miaka 40.Raila alitofautiana na Kibaki katika serikali ya Narc na katika uchaguzi mkuu wa 2007 akaunda kikosi imara kilichojumuisha William Ruto, Musalia Mudavadi miongoni mwa wengine kuunda ODM.
Walidai kwamba walishinda uchaguzi ambao ulifuatiwa na ghasia mbaya zaidi za kisiasa nchini mwaka wa 2008 ambapo watu zaidi ya 1300 waliuawa na maelfu kupoteza makao.
Ghasia hizo ziliisha ilipounda serikali ya muungano akiwa akiwa waziri mkuu Kibaki akihudumu muhula wa pili na wa mwisho. Alikuwa katika nafasi nzuri ya kurithi Kibaki kama rais lakini katika uchaguzi wa 2013 akiwa mgombeaji wa muungano wa Coalition For Restoration of Democracy (CORD) alishindwa na Uhuru Kenyatta ambaye aliungana na William Ruto katika muungano wa Jubilee ulioleta pamoja vyama vyao vya The National Alliance (TNA) na United Republican Party (URP).
Katika Cord, Raila alikuwa na Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper kama mgombea mwenza wake na Moses Wetang’ula wa chama cha Ford Kenya ambao waliungana tena katika uchaguzi mkuu wa 2017 chini ya muungano mpana wa NASA uliojumuisha Musalia Mudavadi miongoni mwa vigogo wengine.
Raila aliwashawishi wenzake wamuunge mkono kuwa mgombea urais wa NASA, kwa ahadi kuwa angehudumu kwa muhula mmoja na kumuunga mmoja wao. Inasemekana alikubali kutimiza ahadi hiyo hata wakishindwa.
Walishindwa na Uhuru Kenyatta aliyekuwa akitetea kiti cha urais japo uchaguzi huo ulifutwa na Mahakama ya Juu iliyoagiza urudiwe. Raila alikataa kushiriki uchaguzi wa marudio.Miezi michache baadaye, Machi 18 2018, alikasirisha vinara wenzake kwa kuzika tofauti zake na Uhuru bila kuwahusisha.
Wadadisi wanasema Raila alichukua hatua hiyo kwa sababu alifahamu wenzake katika upinzani, Musyoka, Musalia, na Wetang’ula hawangemuunga mkono kufuatia mtindo wake wa kushindwa katika kila uchaguzi.
“Raila alijua wazi kuwa ingekuwa vigumu kwake kuungwa mkono na wenzake katika uchaguzi wa 2022 kwa sababu walikuwa na makubaliano kwamba angeunga mmoja wao. Ilitukia kwamba Uhuru naye alitaka mtu wa kumzima William Ruto aliyekuwa naibu wake. Ilibidi Raila achangamkie Uhuru ili kuokoa nyota yake kisiasa katika uchaguzi mkuu wa 2022,” asema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
Anasema ni Uhuru aliyemsaidia Raila kuokoa nyota yake kwa kuunda Azimio la Umoja na kushawishi vyama zaidi ya 22 kujiunga nao. “Kama ilivyotarajiwa, Raila alipoteza Wetang’ula na Mudavadi waliojiunga na Ruto kuunda Kenya Kwanza na ikabidi Uhuru atumie weledi kumshawishi Musyoka na Martha Karua kumuunga Raila.
Hata baada ya kuungwa na Rais aliyekuwa mamlakani, Raila hakufaulu,” aeleza Dkt Gichuki.Baada ya kujinasua na ‘mikosi’ ya Raila, Musalia na Wetang’ula wako serikalini huku Musyoka na wengine waliomuunga waziri mkuu huyo wa zamani wakiwa kwenye baridi.
Wadadisi wanasema kuendelea kushindwa kwa Raila katika uchaguzi ambao huwa anatarajiwa kushinda kunachangiwa na makosa katika mikakati yake hasa anavyohusiana na washirika wake, mfumo wa siasa za Kenya unaokitwa katika ukabila au mikosi ya kawaida ambayo ni yeye binafsi anayeweza kuondoa.
“Sio mara moja Raila ameonekana kukaribia kutwaa mamlaka lakini anakosa dakika ya mwisho. Japo yeye sio kiongozi wa kwanza ulimwenguni kuwa katika hali hiyo, kuna makosa ambayo anapaswa kurekebisha hasa anavyohusiana na washirika wake na wafuasi hasa anaotumia kumwaga damu wakiandamana akiwaita baada ya uchaguzi,” asema mchambuzi wa siasa Jairus Okemwa.
Anatoa mfano wa ukuruba wake wa sasa na Rais Ruto ambao alianzisha bila muafaka na vinara wenza katika Azimio akisema ‘baadhi ya mikosi ni ya kujitakia.”Rais Ruto aliunga azma ya Raila ya kuwa mwenyekiti wa AUC ambayo iligonga mwamba wiki jana.
Leave a Reply