Hussein ana kibarua FKF kurejesha mnato wa soka nchini – Taifa Leo


HUSEIN Mohamed ndiye kinara wa shirikisho la soka nchini FKE na anaingia afisini kukiwa na changamoto chungu nzima za kulemaza soka nchini.

Hussein anatakiwa kubadilisha sera na sura ya FKF kutoka kwa ile ya msururu wa kashfa hadi shirikisho kubalifu ndani na nje ya Kenya. Anatakiwa afikirie namna ya kuhakikisha timu ya taifa Harambee Stars inanawiri na kuzima hii mizozo inayotokana na kukosa kuwalipa ujira wao makocha wa timu ya taifa na kuichia Kenya sifa mbaya

Sijawa mzee wa kusahau mambo kwa hiari ama shuruti. Lakini tangu nilipoelewa soka vizuri, viongozi wa FKF walikuwa wa hadhi kubwa hata wakati shirikisho hilo halikuwa na fedha za kujipiga kifua kama wakati huu. Job Omino angekohoa mapema ya miaka ya tisini, ungefahamu yupo kiongozi. Peter Kenneth aliposhika ngazi 1996 mashabiki wa soka walikubali kazi lifanyika. Sasa tunamtaka Hussein ataayeoneana kwa hoja na vitendo.

Inajulikana kuwa Hussein anapoingia uongozini tayari bundi amelilia kwa ngome yake. Kwanza, Kenya imepoteza fursa ya kuandaa mashindano ya kombe la mataifa barani Afrika mwaka ujao kwa kukosa kutimiza matakwa ya shirikisho la soka Afrika CAF. Rwanda wametunikiwa fursa hiyo kutokana na ubora wa viwanja vyake. Kasarani na Nyayo zetu zinadhaniwa na wakuu wa viwango kuwa nyuga za vijijini. Watangulizi wa Hussein walikuwa wameahidi kutimiza masharti hayo ila hilo halikutimia. Awe mtu wa kusema na kutenda. Asiwe mraibu wa msamiati wa “tumepanga, tutatenga na tumeweka mikakati.”

Mojawapo ya masuala muhimu aliyoweka katika manifesto yake ni kushirikiana na wachezaji wa zamani wa soka na kuhakikisha kuna mfuko wa kulinda masilahi yao. Hii ni hoja komavu inayostahili uzingativu wa kina. Kenya kuna majina makubwa ya wanasoka kama vile Mahamoud Abbas ama ‘Kenya One’ ambaye alikuwa mlinda lango wa haiba kubwa. Baadhi hawajui jinsi bwana huyo alivyokuwa akinyaka mpira kama komba na kuifaa Kenya na AFC Laeopards kwa dhati katika miaka hiyo ya zamani.

Wapo wachezaji wengine ambao wanapitia hali ngumu na wanafia kwa mazingira ovyo sana licha ya kuisaidia Kenya katika michuano ya zamani. Wachezaji hao inawezekana misuli yao ni hafifu; baadhi hawawezi kukimbia hata mita hamsini ila siku zao walichuana na nyasi. Kuna kitu wanachoweza kushauri. Tuwafanye mabalozi wa FKF na soka nchini jinsi yanavyofanya mataifa ya nje. Ndio sababu bado unasikia majina kama Maradona, Pele, Romario na Bebeto wa Brazil.

Hussein ana bahati naibu wake alisukuma ngozi ya kulipwa Parma na Inter Millan. Anaelewa haya mambo ya kuyanadi majina ya wanasoka hata wanapostaafu. Kazi kwake, tunataka FKF yenye maono



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*