MAZISHI ya mamake Spika wa Bunge la kitaifa Moses Wetang’ula, Bi Anna Nanyama Wetang’ula, yaliyofanyika katika eneo la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma yaligeuka kuwa mkutano wa kurushiana lawama kuhusu utekaji nyara.
Katika hafla hiyo, Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa na Gavana wa Kaunti ya Trans – Nzoia Bw George Natembeya, walirushiana cheche kuhusu utekaji nyara mbele ya Rais William Ruto.
Gavana Natembeya alimtaka Rais William Ruto kukomesha utekaji nyara huo, huku akikosoa baadhi ya viongozi aliodai wanahusika na hali hiyo.
Alimtaka Rais kutoa suluhu la haraka akisema kuwa pia yeye ni miongoni mwa viongozi ambao wanapokea matusi mitandaoni kutoka kwa umma.
“Mitandao ya kijamii matusi ni mengi. Kwenye ukurasa wangu, ninapochapisha taarifa, kati ya maoni kumi kutoka kwa wanamitandao, nane ni matusi,” alisema Bw Natembeya.
Kiongozi wengi katika Bunge la Kitaifa Bw Kimani Ichungwa, alikubali kuwa visa vya utekaji nyara vinaendelea kukithiri nchini lakini akamnyooshea kidole cha lawama aliyekuwa Naibu wa Rais kwa kuhusika katika utekaji huo.
“Mheshimiwa Rais, sisemi hakuna utekaji nyara. Gavana Natembeya, iwapo unajua watu ambao wanateka nyara, wewe ni afisa wa zamani wa utawala, umekuwa kamishna wa eneo, peana habari kwa idara ya DCI wachunguze wale wanateka watu,” alisema kwa hamaki.
“Usije hapa kukemea watu. Ulikuwa kamishna wa eneo la Bonde la Ufa wakati mamia ya watu walikuwa wakitekwa nyara na kuuawa eneo la Kerio Valley na kutupwa Mto Yala, wewe ukiwa kamishna wa eneo la Bonde la Ufa. Kwani siku hiyo haukujua maisha ya wananchi ni muhimu?” alihoji Bw Ichungwa.
Mbunge huyo aliapa kuwa atatangaza wazi viongozi wanaoshiriki kwenye utekaji huo.
“Yule ambaye alikuwa kiongozi wako aliyekuwa Naibu wa Rais ndiye mshirika wa utekaji nyara. Anafanya vile ili ionekane ni Rais Ruto,” alidai Bw Ichungwa.
Bw Ichungwa, hata hivyo hakutoa idhibati na hatua wanazopanga kumchukulia Bw Gachagua kwa uhalifu huo ambao umezua simanzi kwa familia za waathiriwa, pamoja na kuleta hali ya taharuki miongoni mwa Wakenya wengi.
Katika hafla hiyo, Rais Ruto aliwataka viongozi mbalimbali kuepuka mizozo kwenye hafla za mazishi ambazo huhudhuria na viongozi kutoka nchi zingine.
Aliwataka viongozi hao kutofautiana kwa njia inayofaa bila kuchochea chuki kwa wananchi.
“Kuna wale wageni wamefika hapa, wanashangaa kuona cheche kwenye hafla kama hii. Hili ndilo taifa ninaloongoza…Tafadhali, demokrasia ni kitu kizuri sana na lazima tuwe na mipaka. Mataifa mengine yanatuangalia na washikadau mbalimbali,” alihimiza Rais Ruto.
Leave a Reply