IG Kanja asema atafika kortini wiki ijayo – Taifa Leo


INSPEKTA JENERALI  wa Polisi, Douglas Kanja, amesema atafika mahakamani wiki ijayo kuhusiana kesi ya kutekwa nyara na kutoweka kwa vijana.

Akizungumza baada ya kuhudhuria kongamano la Maafisa wa Polisi wa Utawala  kutoka maeneo yote nchini huko Diani, Bw Kanja alisema kuwa uchunguzi kuhusu watu waliopotea uko katika hatua za juu na amemwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuchukua hatua zifaazo.

“Hakuna shida yeyote, wakati wa kufika kortini, mimi mwenyewe nitafika binafsi,” Bw Kanja alisema.

Alisema kuwa ametoa maagizo kwamba uchunguzi ufanywe kwa kina na wahusika wote wakamatwe kulingana na sheria.

Bw Kanja alikuwa amekosolewa kwa kutofika mahakamani licha ya kuitwa kutokana na ongezeko la visa vya utekaji nyara  nchini.

Siku nne zilizopita, Bw Kanja na Mkuu wa DCI, Amin Mohammed, walikosa kufika mahakamani  katika kesi inayohusu watu watatu waliotekwa nyara huko Mlolongo.

Jana, Bw Kanja alifafanua kuwa yeye anaheshimu sheria na atajiwasilisha mahakamani  Januari 27.

“Kama Inspekta Jenerali, sina sababu yoyote ya kutoheshimu mahakama kama inavyotakiwa na sheria. Kwa hivyo, tarehe 27 nitaenda mahakamani kama nilivyoagizwa na Mahakama Kuu,” alisema.

Akizungumza katika mkutano huo, Bw Kanja aliwapongeza polisi kwa kudhibiti maandamano tangu Juni 2024 walipokumbana na changamoto kubwa.

Wakati huo huo, alisema polisi wanajitahidi kurejesha imani ya umma, huku wakitumia teknolojia na zana za kidijitali kuongeza ufanisi wao.

“Kuanzia Aprili mwaka huu, tutaanza utekelezaji wa Kitabu cha Matukio cha kidijitali (OB). Hii itawawezesha yeyote mwenye simu ya kisasa kutoa ripoti popote walipo,” alisema, akiongeza kuwa polisi watafuatilia ripoti hiyo.

Pia, Bw Kanja alisema huduma nyingine kadhaa za polisi pia zitatolewa kupitia mfumo huo wa kidijitali.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*