GAZA, PALESTINA
ISRAEL Alhamisi iliendeleza mashambulizi yake Gaza saa chache tu baada ya muafaka wa kusitisha vita kwenye ukanda huo kuafikiwa.
Utawala wa Palestina ulithibitisha watu 46 waliuawa jana kutokana na shambulizi la Israel.
Mnamo Jumatano usiku, mazungumzo ambayo yamekuwa yakisimamiwa na Qatar, Misri na Amerika yalizaa matunda baada ya Israel na Hamas kuafikiana kusitisha vita kuanzia Juampili hii.
Mkataba huo unapisha kuwaachiliwa kwa mateka ambao wamekuwa wakizuiliwa na Hamas huku Israel nayo ikiwaachilia Wapalestina ambao wamekuwa wakisota kwenye magereza yao.
Pia maafikiano hayo yanatoa mwanya wa wiki sita wa kusitishwa kwa mapigano huku Israel nayo ikiyaondoa majeshi yake kwenye ukanda wa Gaza.
Jana, wapiganiaji ukanda wa Gaza walirusha roketi upande wa Israel lakini hakuna mauaji ambayo yalitokea. Israel ililipiza kisasi na kuwaua zaidi ya Wapalestina 46.
Akizungumza Doha, Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohamed bin Abdulrahman Al Thani alisema kuwa baada ya kusitishwa kwa vita kuanzia Jumapili, yaliyomo kwenye mkataba huo yataanza kutekelezwa mara moja.
“Vita vitasitishwa Gaza, Wapalestina ambao wanahitaji msaada wa kibinadamu watafikiwa na mateka nao wataungana na familia zao baada ya kuzuiliwa kwa kipindi cha zaidi ya miezi 15,” akasema Rais wa Amerika Joe Biden akiongea baada ya muafaka huo kuafikiwa.
Rais Mteule Donald Trump ambaye anatarajiwa kuchukua rasmi uongozi mnamo Jumatatu alidai kuwa ndiye alichangia pakubwa kuafikiwa kwa mkataba huo.
Ingawa hivyo, lazima baraza la mawaziri Israel pamoja na serikali iidhinishe muafaka huo ndipo izingatiwe kuwa wameikubali rasmi. Kura kuhusu hilo ilitarajiwa kupigwa baadaye hapo jana na ilitarajiwa kupita japo kuna wengine ambao wamekuwa wakiupinga kwenye utawala wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Katika mitandao ya kijamii, baadhi ya wenyeji wa Gaza waliitaka Palestina iwe makini na mienendo ya Israel. Wanadai Israel huenda ikaendeleza uvamizi na kutekeleza mauaji mnamo leo na kesho kabla ya makubaliano kuanzia Jumapili.
Ingawa hivyo, makubaliano hayo yalisherehekewa sana Wapalestina Gaza, ukanda ambao umekuwa ukikumbwa na ukosefu wa chakula, maji, makao na mafuta.
Katika mji wa Khan Younis ambako Israel imekuwa ikiendeleza mapigano makali, sherehe zilitanda huku Wapalestina wakipeperusha bendera zao na kusakata ngoma.
Jijini Tel Aviv, familia za Waisraeli ambao walikuwa wametekwa walifurahi, wakisema hatimaye watakuwa wakiungana na wapendwa wao.
Vita hivyo vilianza mnamo Oktoaba 7, 2023 baada ya Hamas kuvamia Israel na kuwa raia 1,200 huku wakiwateka wengine 250. Israel nayo imewaua zaidi ya Wapalestina 46,000 kwa kipindi cha miezi 15.
Leave a Reply