VIKOSI vya Israel Ijumaa vilivamia hospitali ya Kamal Adwan, mojawapo ya vituo vitatu vya matibabu kaskazini mwa ukingo wa Gaza, na kuamuru mamia ya wagonjwa kuondoka na kuchoma moto sehemu yake, maafisa wa wizara ya afya walisema.
Kwingineko huko Gaza, mashambulizi ya Israel yameua takriban watu 25, wakiwemo watu 15 katika nyumba moja katika mji wa Gaza, madaktari na idara ya huduma ya dharura ya raia ilisema.
Wizara ya afya ya Palestina ilisema mawasiliano na wafanyikazi ndani ya hospitali ya Beit Lahiya, ambayo imekuwa ikizingirwa na vikosi vya Israeli kwa wiki, yamepotea.
Baadaye Ijumaa, wizara ya afya huko Gaza ilisema kwamba vikosi vya Israeli vilimkamata mkurugenzi wa hospitali, Abu Safiya, na wafanyikazi wake kadhaa.
“Vikosi vya uvamizi viko ndani ya hospitali sasa na vinaiteketeza,” mkurugenzi wa wizara Munir Al-Bursh alisema katika taarifa.
Jeshi la Israel lilisema lilijaribu kupunguza madhara kwa raia na “liliwezesha uhamishaji salama wa raia, wagonjwa na wafanyikazi wa matibabu kabla ya operesheni,” lakini haikutoa maelezo.
Katika taarifa yake, ilisema wapiganaji wa kundi la Hamas la Palestina, ambalo hapo awali lilikuwa likidhibiti Ukanda wa Gaza, walikuwa wakijificha katika hospitali hiyo wakati wote wa vita na wamefanya eneo hilo kuwa ngome muhimu.
Hamas ilipuuzilia mbali kauli hiyo kama ya “uongo,” ikisema hakukuwa na wapiganaji katika hospitali hiyo.
Youssef Abu El-Rish, naibu waziri wa afya aliyeteuliwa na Hamas, alisema vikosi vya Israel vimechoma moto idara ya upasuaji, maabara na ghala.
Jeshi la Israel (IDF) lilisema kulikuwa na moto mdogo katika jengo tupu ndani ya hospitali hiyo ambao ilisema ulikuwa umedhibitiwa.
“Kuhusu madai kwamba moto huo ulisababishwa na milio ya risasi ya IDF, IDF kwa sasa haifahamu tukio lolote kama hilo,” ilisema.
Kama hospitali za Indonesia na Al-Awda, Kamal Adwan imeshambuliwa mara kwa mara na vikosi vya Israeli ambavyo vimekuwa vikishambulia kaskazini mwa ukingo wa Ukanda wa Gaza kwa wiki, wafanyikazi wa matibabu wa Palestina wanasema.
Bursh alisema jeshi lilikuwa limeamuru watu 350 kuondoka Kamal Adwan kwenda shule ya karibu inayohifadhi familia zilizohamishwa.
Abu El-Rish alisema wanajeshi walikuwa wakihamisha wagonjwa na wafanyikazi wa matibabu katika Hospitali ya Indonesia, ambayo tayari iliharibiwa na vikosi vya Israeli.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply