Jinsi Hussein alivumilia mahangaiko ya FKF kuteuliwa rais mpya wa kandanda nchini – Taifa Leo


RAIS mpya wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Hussein Mohamed alivuka vizingiti si haba kabla ya kufanikiwa kutimiza azma yake kutwaa usukani wa soka.

Hussein, 47, alitwaa usukani mwa FKF baada ya kupata kura 67 huku Makamu wa Rais wa FKF anayeondoka Dotris Petra pamoja na katibu wa zamani Barry Otieno wakipata kura moja moja kwenye duru ya pili ya uchaguzi huo ulioandaliwa Desemba 7, 2024 katika ukumbi wa Kasarani jijini Nairobi.

Licha ya Petra na Otieno kusalimu amri baada ya mkondo wa kwanza, ilibidi mkondo wa pili uandaliwe ili kuhakikisha mwaniaji anapata asilimia 50 za kura zote 90 zilizopigwa.

Hussein Mohammed (kushoto) akipongezwa na mpinzani Barry Otieno baada ya kuchaguliwa rais mpya wa FKF katika ukumbi wa Kasarani, Nairobi, hapo Desemba 7, 2024. PICHA | CHRIS OMOLLO

Hii ilikuwa mara ya pili kwa Mohamed kuwania urais wa FKF baada ya kuangushwa na Sam Nyamweya mwaka 2011, wakati huo akiwa na umri wa miaka 34 pekee.

Hata hivyo, safari ya urais haijakuwa rahisi kwa Mohamed, ambaye pia ni Naibu Mwenyekiti wa klabu ya Murang’a Seal inayoshiriki Ligi Kuu (KPL).

Mwezi Januari aliaibishwa na hata karibu aangushiwe kipigo na kufurushwa uwanja wa Raila Odinga katika Kaunti ya Homa Bay.

Alikumbana na aibu hiyo alipohudhuria fainali ya kipute cha Genowa ambacho kinadhaminiwa na Gavana Gladys Wanga wa Homa Bay.

Uhusiano wake mbovu na uliokuwa uisimamizi wa FKF ulitokeza wazi baada ya marefa kuambiwa wasiendeshe fainali hadi atoke ugani.

Hussein Mohammed (kushoto) akipongezwa na rais wa FKF anayeondoka Nick Mwendwa baada ya kushinda uchaguzi huo. PICHA | CHRIS OMOLLO

Aliyekuwa mwenyekiti wa FKF Homa Bay, Maurice Obweno, ambaye ni mshirika wa Rais Nick Mwendwa anayeondoka alijaribu hata kumwondoa Mohamed lakini Wanga akaingilia kati na baadaye rais huyo mpya akaruhusiwa kuhudhuria fainali.

Mwendwa na kundi lake waliendelea kumuandama Mohammed huku Otieno mnamo Machi 17 akitumia Murang’a Seal barua ya kukataa Mohamed awakilishe timu hiyo mkutano wa mwisho wa mwaka wa FKF.

Suala hilo lilizua majibizano makali huku Mwenyekiti wa Murangá, Robert Macharia, akishutumu FKF na kusema haiwezi kuamulia klabu wawakilishe kwenye kikao hicho, ambacho kiliishia kutofanyika kwa amri ya mahakama.

Masaibu dhidi ya Mohammed hayakukomea hapo. Kulikuwa na hila ya kuwazuia wandani wake kuwania katika matawi ya shirikisho.

Hussein Mohammed (kushoto) na mgombea mwenza McDonald Mariga walipozindua kampeni yao ya urais wa FKF mnamo Oktoba 12, 2024 mjini Nairobi. PICHA | CHRIS OMOLLO

Baada ya bodi kuchapisha orodha ya wawaniaji wa kura katika matawi, ilibidi mrengo wa Mohammed uelekee Mahakama ya Kutatua Mizozo ya Michezo (SDT) ili kuhakikisha wanakubaliwa kushiriki.

Mfano ni kaunti za Trans Nzoia na Mombasa ambapo Isaac Munene na Alamin Abdallah mtawalia walizuiwa kuwania uenyekiti lakini wakarejeshwa na SDT na hata kuibuka washindi.

Vile vile, wakati wawaniaji urais walipeleka karatasi zao kwa Bodi ya Uchaguzi mwezi Oktoba, wengi walibashiri Mohammed hangeshiriki kwa kutohitimu lakini mwishowe ametamba tena kwa kra nyingi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*