MAELEZO yameibuka kuhusu jinsi polisi walivyopuuza dalili za ghasia za kisiasa katika mazishi ambayo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alilazimika kutoroka kuokoa maisha yake baada ya kushambuliwa mnamo Alhamisi.
Wenyeji wamefichua kuwa mpango wa kumshambulia Bw Gachagua ungetekelezwa siku moja kabla ya mazishi.
Duru zinasema kuwa awali kundi la vijana lilipangwa kutekeleza shambulizi hilo Jumatano baada ya habari kusambazwa kwamba Bw Gachagua angetembelea familia hiyo kutoa mchango wake binafsi na kuhudhuria kikao cha maombi ya jioni.
Bw Gachagua, kupitia kwa mmoja wa washirika wake wa karibu, alituma mchango wake wa kibinafsi wa Sh50,000 kwa familia baada ya kamati ya kuandaa mazishi kumuomba asaidie.
Bw Gachagua pia alieleza nia yake ya kuhudhuria mazishi hayo. Haya ni kulingana na Joseph Karanja Muchai almaarufu Shujaa ambaye alikuwa sehemu ya kamati iliyoandaa mazishi.
Duru za polisi
Chanzo kikuu cha polisi kilifichua kwa sharti tusitaje jina kwamba walikuwa na taarifa za kijasusi kuhusu uwezekano wa fujo kutokea kutokana na matukio ya awali baada ya Bw Gachagua kutimuliwa ofisini.
Hata hivyo, alidai kuwa watu serikalini walitumia ushawishi wao kuwaonya maafisa wakuu wa polisi dhidi ya kutoa usalama kwa hafla ya Bw Gachagua.
Inasemekana kuwa wahuni hao walisafirishwa hadi eneo la Bibirio-ini, eneo la mazishi kutoka Kabete, Kikuyu, Limuru na Kiambaa. Walianza kuwasili kuanzia saa nane asubuhi hata kabla ya msafara kutoka chumba cha kuhifadhia maiti kufika.
Masimulizi ya mashahidi yanaonyesha jinsi vijana hao ambao wanakijiji wanasema hawakuwa wa eneo hilo, walivyokuwa wakivuta sigara baada ya kufika na kuketi karibu na jukwaa la watu mashuhuri.
Baadaye walizua vurugu wakirusha mawe kwenye jukwaa kuu kabla ya kuangusha mahema hayo na kutumia viti, fimbo na kila aina ya silaha, kushambulia msafara wa Bw Gachagua na washirika wake wa karibu wa kisiasa.
“Nitakuwa nasema uwongo nikikuambia kuwa hatukuwa na habari za ujasusi kwamba fujo zingezuka wakati wa mazishi hayo. Taarifa na vidokezo vyote vilikuwa wazi na baadhi ya wasimamizi wa eneo hilo ambao wako kwenye vikundi vya WhatsApp kama vile Uteti wa Limuru(Siasa za Limuru) walitufahamisha.
Uteuzi wa kisiasa
“Utafanya nini watu walio karibu na mamlaka wakikuita wewe na maafisa wengine wakuu wa polisi na kukuambia usitoe usalama kwa fulani, yeye si afisa wa serikali tena. Utafanya nini? Unajua uteuzi wa maafisa wakuu wa polisi ni wa kisiasa na unajua maafisa wa polisi wanalalamika kimya kimya.”
“Ndiyo, tunajua kipi kibaya na kipi ni sahihi lakini cha kusikitisha ni kwamba wakati mwingine tunaingia kwenye mapigano ambayo si yetu na kwa viwango vya kibinafsi unahisi unawaangusha watu na kutumiwa vibaya kwa sababu pamoja na hayo yote wanateseka moja kwa moja,’’ maafisa wa polisi waliambia Taifa Leo kwa sharti hatatawataja majina wakihofia kudhulumiwa na kuhamishwa mara moja.
Kwa kauli rasmi, maafisa wakuu wa huduma hiyo walikanusha kufahamu mipango ya ghasia hizo huku Bw Mohammed Amin, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Ijumaa akilaumu ukosefu wa ujasusi wa awali kuhusu shambulio dhidi ya Bw Gachagua.
“Tukio la Alhamisi Limuru linachunguzwa na hatua zitachukuliwa dhidi ya wahusika na wachochezi. Hatukuwa na taarifa za kijasusi kuhusu shambulio lolote lililopangwa,” Bw Amin aliambia Taifa Leo.
Katika drama zaidi, aliyekuwa Mbunge wa Limuru, Peter Mwathi na MCA wa Wadi ya Bibirioni, Christopher Ireri walidai kuwa walitekwa nyara katika eneo la tukio, wakawekwa kwenye magari aina ya Subaru, wakazungushwa na baadaye kutupwa karibu na mji wa Ruiru.
Bw Amin alishauri wahusika wote kukoma kutoa madai ambayo hawajaripoti rasmi katika vituo vya polisi.
Ripoti kwa polisi
“Ikiwa unadai ulitekwa nyara, tafadhali toa taarifa katika kituo cha polisi ili tuwape wachunguzi. Iwapo uliona washambuliaji au una kidokezo kingine chochote muhimu cha kutusaidia kuwanasa wahalifu, turuhusu tuipate kwa ujasiri. Tunasalia kuwa taasisi isiyopendelea upande wowote,” akasema Bw Amin.
Bw Gachagua alikuwa akihudhuria mazishi ya Erastus Nduati, 23, almaarufu Mwene Limuru (mmiliki wa Limuru).
Bw Nduati alifariki baada ya kakake kuamka asubuhi moja na baada ya ugomvi wa muda mfupi mapema wiki jana, alimkata na kumuua kwa panga.
Bw Nduati alizikwa haraka huku waombolezaji wakitaka kutafuta usalama na familia ililazimika kuwasihi warudi kusaidia kuteremsha jeneza. Zaidi ya hayo, familia inalazimika kulipa zaidi ya Sh100,000 baada ya viti ilivyokodisha kuharibiwa na wakora hao.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply