WAZIRI wa Madini, Uchumi wa Baharini na Masuala ya Ubaharia, Bw Hassan Joho, ameonekana kuchukua usukani wa kuwa mtetezi sugu wa Rais William Ruto na serikali yake eneo la Pwani.
Wakati wa ziara ya rais katika Kaunti ya Taita Taveta iliyoanza Jumatatu, Bw Joho alisema ingawa hatarajiwi kujihusisha kwa siasa akiwa waziri, hatasita kuwakashifu wanaopinga serikali bila sababu.
Gavana huyo wa zamani wa Mombasa aliwapuuzilia mbali watu ambao hukosoa serikali kwenye mitandao ya kijamii, akidai kuwa hali mashinani ni tofauti na ile inayoenezwa mitandaoni.
“Nakuhakikishia (rais) hapa kwetu tutashikana na wewe katika safari ya kuunganish Wakenya. Mimi Hassan Joho ni waziri wa William Samoei Ruto,” akasema, katika mikutano ya hadhara iliyofanyika maeneo tofauti ya Taita Taveta mnamo Jumatatu.
Bw Joho alikuwa miongoni mwa wanachama wa ODM ambao walichaguliwa kuwa mawaziri katika serikali ya Bw Ruto, wakati ambapo serikali inampigia debe kinara wa chama hicho, Bw Raila Odinga, kuwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).
Ushirikiano huu kati ya ODM na Kenya Kwanza uliwafanya viongozi wa ODM kuanza kuitetea serikali ambayo awali walikuwa wakiikosoa vikali kwa hatua zilizokuwa zikionekana kwenda kinyume na matarajio ya wananchi.
Katika siasa za Pwani, Bw Joho, ambaye alikuwa naibu kiongozi wa ODM kabla apewe kazi ya uwaziri, ni mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa.
Mbali na Bw Joho, wengine walio na ushawishi katika siasa za ukanda huo ni Spika wa Seneti, Bw Amason Kingi, na Waziri wa Viwanda, Bw Salim Mvurya ambao pia ni magavana wa zamani wa Kilifi na Kwale mtawalia.
Bw Kingi alisema rais ashaonyesha nia ya kudumisha umoja nchini na hilo linafaa kuigwa na viongozi wote.
“Rais alichaguiwa kwa UDA lakini akaleta viongozi wote pamoja. Hii ni kwa sababu ya juhudi zake kuleta taifa lote pamoja. Hatutaki tena kuwa na Wakenya wanaovumilia kuwa Wakenya, wote lazima wajivunie kuwa Wakenya,” akasema.
Wakati wa ziara hiyo, Gavana wa Taita Taveta, Bw Andrew Mwadime, alimtaka rais ahakikishe kuwa wakazi wananufaika na mapato ya Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo.
Rais alisema nakala ya makubaliano ya pamoja kuhusu suala hilo iko tayari na itatiwa sahihi na serikali ya kitaifa na kaunti mapema mwaka ujao.
Leave a Reply