KUNA haja ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuweka mfumo wa kutumia Ziwa Victoria ili kuzuia unyanyasaji wa wavuvi ndani ya ziwa hilo, Waziri wa Madini, Uchumi wa Majini na Masuala ya Baharini Hassan Ali Joho, amesema.
Bw Joho alisema ziwa hilo hutumiwa na nchi kadhaa na ni kupitia mfumo kama huo ambapo nchi za Afrika Mashariki zinaweza kulitumia bila mizozo.
Visa vya wavuvi wa Kenya kunyanyaswa na kupoteza maisha mikononi mwa maafisa wa usalama wa Uganda vimekuwa vikiendelea kwa miaka mingi huku kilio cha wavuvi hao kwa serikali iwasaidie kikipuuzwa.Bw Joho alisema serikali itatumia mamlaka yake kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupata suluhu la kudumu kuhusiana na zogo hilo.
Alifichua kwamba atamtembelea mwenzake wa Uvuvi wa Uganda kujadili jinsi ya mfumo wa kutumia ziwa hilo unaweza kubuniwa kwa kushirikisha nchi nyingine za Afrika Mashariki.
“Nitaenda huko kwa heshima kuu na unyenyekevu kujadiliana na mwenzangu jinsi tunaweza kupata suluhu ya kudumu la suala hili. Hakuna nchi inafaa kunyanyasa wavuvi wa nchi nyingine,” alisema.
Bw Joho alikuwa akizungumza alipozuru maeneo ya kutua samaki katika kaunti ndogo za Bondo na Rarieda ambako alisema serikali itaweka vifaa vya kuhifadhi samaki katika Usenge, Wichlum na Kamito ili kuinua biashara ya uvuvi katika eneo hilo.
Leave a Reply