Juhudi za Ruto kusaidia wanamuziki kunufaika na ubunifu na jasho lao – Taifa Leo


RAIS William Ruto ameagiza Bodi ya Hakimiliki ya Kenya kubuni mfumo wa kufuatilia ukusanyaji na ugavi wa mirahaba kwa wanamuziki na wasanii.

Kwa kushirikiana na wadau wengine wa tasnia na jukwaa la eCitizen, Dkt Ruto alisema, Bodi ya Hakimiliki ya Kenya (KECOBO) “lazima ianzishe mfumo wa uwazi, wa wakati halisi wa kukusanya na kusambaza mrabaha kwa wamiliki halali,”

KECOBO, lililoanzishwa chini ya Sheria ya Hakimiliki ndilo shirika la udhibiti lililo na mamlaka ya kusimamia ulinzi na ukuzaji wa hakimiliki na haki zinazohusiana nchini Kenya.

Bodi huwezesha usajili wa hakimiliki, kupinga ukiukaji, na kuongeza ufahamu kuhusu haki miliki.

Dkt Ruto anatumai kukomesha kile alichotaja kama ukosefu wa haki katika usambazaji wa mrabaha katika  ubunifu kwa hatua hiyo kali.

Alikuwa akizungumza wakati wa maadhimisho  ya 61 ya Jamhuri Day jijini Nairobi aliposema “haikubaliki” kwamba mafanikio ya wasanii na waigizaji katika maeneo ya ubunifu kuhujumiwa.

“Haikubaliki kuwa msanii kupata kiasi kidogo cha Sh10,000 kwa mwaka huku wale walio na jukumu la kukusanya mirabaha yao wakiweka mfukoni mamilioni kila mwezi. Udhalimu huu lazima ukomeshwe,” Rais Ruto aliagiza.

Wanamuziki, alisema, ni mapigo ya moyo na roho ya utamaduni wa nchi lakini kwa muda mrefu wamenyimwa mapato yao halali.

“Ninawapongeza wasanii katika nafasi zetu za ubunifu ambao kazi yao inaleta uhai katika miji, mitaa na runinga zetu, lakini mafanikio yao yamegubikwa na ukosefu wa haki.”

Wakati huo huo, Dkt Ruto alisema nchi inajitayarisha  kwa zabuni ya kuandaa Kongamano la Ulimwenguni la Ubunifu wa Uchumi wa 2026.

“Kuandaa kongamano hili kutakuwa tamko la kijasiri la uongozi wa Kenya katika uchumi wa ubunifu,” Rais Ruto alisema, akiongeza kuwa hiyo pia inaashiria kujitolea kwa nchi kusherehekea talanta na kuonyesha utamaduni wake mzuri kwa ulimwengu.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*