KATIKA kitongoji cha Soweto, Kayole, Kaunti ya Nairobi, kundi moja la wafugaji kuku lina hadithi ya kuvutia jinsi lilivyoanzishwa.
Joyful Birds Self-Help Group, kundi la wanachama 21, liliasisiwa miaka kumi iliyopita kupitia wanamemba wanaokiri waliunganishwa na jukwaa la fitina.
Soweto, ni mojawapo ya vitongoji duni Nairobi na wanachama hao ni wenyeji ambao wengi wao hawakuwa na ajira.
Kupitisha muda, walikuwa wakishiriki mazungumzo yaliyosheheni masengenyo.
“Tulianzisha Joyful Birds 2012 tukiwa wanachama wanane, ambao ni wakazi wa Soweto. Wengi wana familia ila hawana kazi. Walikuwa wakipoteza muda kwa kushiriki gumzo la fitina, ila jambo moja lilikuwa wazi; baada ya siku majukumu na bili zilikuwa zikiwasubiri,” anasema Timothy Malasi, Mwenyekiti.
Kulingana Malasi, ni memba watatu pekee walikuwa na ajira, na kila walipotangamana walikuwa wakihurumia wenzao.
Baada ya muda, waliamua kutumia jukwaa la masengenyo kufanya jambo la busara.
Licha ya changamoto zilizowazingira, walikubaliana kuchanga Sh25 kila wiki – kila mhusika.
Jumapili, baada ya ibada ya kanisa Malasi anasema walikuwa wakikutana.
Walichanga kwa muda wa miezi mitatu mfululizo wakiweka hela hizo kama akiba.
“Kila aliyeshiriki mkutano na kuchanga alionekana mtu anayejua anachofanya,” Malasi anakumbuka.
Hatimaye, walitinga Sh5, 000 japo kuamua jambo ambalo wangefanya na pesa hizo ilikuwa kizungumkuti.
“Kumbuka, ni hela za watu waliopambana kukithi familia zao mahitaji muhimu ya kimsingi. Majaribu yalikuwa mengi,” anasema.
Maamuzi yaliafikiwa kupitia kisa cha mmoja wa wanachama aliyekuwa na hafla ya kuombea mwanawe na kuku ilikuwa chaguo la kupikia walioalikwa.
“Wazazi wake kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya na pasta walikuwa wageni mashuhuri, na mila na itikadi za anakotoka nyama za kuku ndizo zinathaminiwa,” Malasi anaelezea.
Mbele na nyuma, mwanachama huyo, Malasi anadokeza kwamba alikuwa na Sh3, 000 na alipozunguka masoko ya Kayole kuku mmoja alikuwa akiuziwa Sh2, 000, hii ikiwa na maana kuwa alikuwa na punguo la Sh1, 000.
Anasimulia kwamba alilazimika kuongeza hela hizo ili anogeshe hafla ya kuombea mwanawe.
“Mahangaiko aliyopitia yalitufungua macho tukaamua kuanzisha mradi wa kuku,” Malasi anadokeza.
Pesa walizoweka akiba, zikawa mtaji ambapo walianza na vifaranga 20, japo tano pekee ndio walifanikiwa kukua hadi wakakomaa.
Malasi anasema walikodi sehemu karibu na Mto Soweto, wakajenga vizimba.
Wanachama kadhaa ni mafundi; seremala na yule wa kuchomelea vyuma.
Miaka 12 baadaye, Joyful Birds Self-Help Group inajivunia kuwa biashara iliyosajiliwa na yenye mashiko; inauza bidhaa za kuku na kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Chuo Kikuu cha Masuala ya Kilimo na Teknolojia (JKUAT) na kile cha Kenyatta (KU), ni kati ya taasisi ambazo wanafunzi wake wanaosomea kozi za kilimo na ufugaji wamenolewa makali na kundi hilo
Wakati wa mahojiano, tulipata likiwa na kuku wapatao 650 idadi hiyo ikiwa ni punguo kutoka 1, 500 baada ya majengo yao kubomolewa Aprili 2024 kufuatia bomoabomoa iliyotekelezwa na serikali kuondoa waliojenga karibu na mito Nairobi.
Ubomoaji huo, uliwasababishia hasara ya mayai 500 ambayo yalikuwa kwenye mashine ya kuotesha na kuangua vifaranga yaliyoharibika.
“Shabaha yetu ilikuwa kufikisha kuku 2, 000. Ubomoaji haukutupa nafasi ya kupanuka,” Malasi anasikitika.
Joyful Birds imewekeza kwenye mitambo ya kuotesha mayai ya idadi jumla ya 1,056 na nyingine 300.
Kwa sasa, wanahudumu kwenye jengo la ghorofa mbili walilokodi ili kufufua biashara yao.
“Tukipata mdhamini atupige jeki, tutaangazia upungufu wa bidhaa za kuku jambo litakalofungua nafasi za ajira hasa kwa vijana,” anasema Mzee Patrick Atetu, mwanachama na mshauri wa mradi huo.
Biashara ya kundi hilo ni kuzua mayai, vifaranga na kuku waliokomaa.
Isitoshe, huongeza thamani vipande maalum vya kuku.
Mradi wao una duka la mayai na kuuza sehemu za kuku, eneo la kusaga chakula, afisi na vizimba kwa mujibu wa umri wa kuku.
Kando na kuku, pia hufuga kanga, bata mzinga na kware.
“Tumekumbatia teknolojia na bunifu za kilimo jijini, na tuna matumaini kufungua matawe mengine nje ya Nairobi,” anasema Elphas Namolo, memba aliyejiunga miaka mitano iliyopita.
Namolo anaendeleza ufugaji mwingine wa kuku, katika boma lake.
Mradi huo hasa ni wa kuku wa kienyeji walioboreshwa wanaojumuisha Sasso, Kuroiler, na Kebro, na vilevile kienyeji halisi.
Bei ya bidhaa zao, inaanzia Sh110 kifaranga wa siku moja hadi Sh2, 500 kuku waliokomaa, hasa jogoo.
Joyful Birds ina uongozi imara, kuanzia afisi ya mwenyekiti na naibu wake, karani, mwekahazina na patroni ambaye si mwanachama.
Kuendeleza uwazi, malipo yoyote hufanywa kwa njia ya simu hela zinaelekezwa kwenye akaunti ya pamoja benkini.
“Yeyote yule anayepokea pesa lazima azitume benki,” anasisitiza Lucy Anyango, naibu mwekahazina.
Kundi hilo huweka rekodi za mauzo, chanjo, ukusanyaji mayai, malisho, uoteshaji mayai, na huduma nyinginezo kwenye biashara yao.
Limeajiri wafanyakazi watatu wa kudumu, ambao ni wanamemba.
Kupunguza gharama ya chakula, hukuza shayiri na kufuga wadudu maalum aina ya Black Soldier Fly (BSF).
“Shayiri hukomaa kwa muda wa siku saba pekee. Matumizi yake pamoja na BSF, yamepunguza gharama kwa karibu asilimia 50,” Zadock Ambuka, karani na msimamizi wa malisho, akaambia Akilimali Dijitali ilipozuru mradi huo.
Faida, hugawana kwa mujibu wa hisa kila memba aliwekeza. Hilo hufanyika mwishoni mwa mwaka, baada ya kufanya mahesabu.
Aidha, wana Katiba inayowaongoza.
“Hela zozote zinazotolewa lazima wanachama wote waarifiwe na zinakopelekwa ama matumizi yake,” Malasi akasema.
Licha ya changamoto wanazopitia, wanakiri mradi huo umewafaa pakubwa, Beatrice Owano, memba, akidokeza kwamba amefanikiwa kusomesha watoto wake watano kuupitia.
Malasi, vilevile anasema mwanachama anayelemewa kulipa karo au kodi ya nyumba kundi hugharamia kisha naye anatoa huduma.
Jitihada zao zimetambuliwa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na pia Chama cha Kilimo cha Kenya (ASK) 2023 ambapo Joyful Birds iliorodheshwa miongoni mwa biashara tatu bora wakati wa maonyesho ya chama hicho Nairobi.
Leave a Reply