IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya, imewashauri Wakenya katika maeneo tofauti nchini kujiandaa kupata mvua ya wastani katika kipindi cha siku tano zijazo, kuanzia Jumamosi, Januari 18 hadi Jumatano, Januari 22.
Katika utabiri wake wa hali ya hewa wa siku tano, idara iliorodhesha maeneo ya Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nyanda za Juu Mashariki, Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ufa Kusini, na nyanda za chini-mashariki (maeneo yanayopakana na Tanzania) kujiandaa kwa mvua mwishoni mwa wiki.
Idara hiyo ilisema katika katika ushauri wake kwamba maeneo yaliyotajwa hapo juu yatapata mvua ya wastani ambayo itanyesha mchana.
Kaunti zinazotarajiwa kupata mvua mwishoni mwa juma ni pamoja na Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, na Trans Nzoia.
Zaidi ya hayo, kaunti za Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia, na Pokot Magharibi zimeorodheshwa kuwa na hali sawa ya mvua.
Vile vile, kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka, na Nairobi zinatarajiwa kupata mvua ya kiwango cha wastani.
Kaunti zingine zinazotabiriwa kupata mvua nyepesi ni pamoja na Kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado, na Taita Taveta, pamoja na sehemu za bara za Kaunti ya Tana River.
Idara ya Hali ya Hewa inatabiri kwamba maeneo mengi ya nchi yatasalia kuwa na jua na ukavu, huku halijoto katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini Mashariki, kama vile Wajir, ikitarajiwa kufikia kiwango cha juu cha nyuzi 37°C katika kipindi hicho.
Leave a Reply