Kadiria uwezo wa mwanao kutumia vifaabebe – Taifa Leo


WATAFITI wa malezi dijitali wamekuwa wakirejelea neno “mlo wa kidijitali” kumaanisha mpango wa matumizi ya vifaa vya kidijitali kwa watoto, sawa na wazazi wanavyowaza kuhusu lishe bora kwa watoto wao.

Teknolojia inalinganishwa na sukari; swali ni, mtoto wako anapaswa kutumia vijiko vingapi vya sukari hii? Wataalamu wanasema jibu linategemea kusudi ya sukari hiyo.

Wanahoji kuwa akili za watoto hukua kutokana na uzoefu, hivyo wanahitaji uangalizi wa makini wakati wa ukuaji huo.“Wazazi wanatakiwa kujua ni muda gani unafaa kwa watoto wao kutumia vifaabebe – iwe ni mitandao ya kijamii, kutazama vipindi kwenye simu au televisheni za kisasa, au gemu za mitandaoni,” alitanguliza Dkt Amanda L. Giordano akiandika katika jarida la Psychology Today.

Kabla ya mzazi kununua gemu yoyote ya mtandao anahimizwa kufanya utafiti wa kina kubaini iwapo inafaa kwa umri wa mwanawe, pamoja na hatari na manufaa kwa mtoto.

“Kumbuka, kinachomfaa mtoto wako wa miaka 12 ni tofauti kabisa na kinachomfaa mtoto mwingine mwenye umri sawia wa jirani yako,” akasema Dkt Amanda.

“Usinunulie mtoto wako kifaabebe eti kwa sababu jirani yako amenunulia mtoto wake wa umri sawa na wako kifaa hicho. Kadiria uwezo wa mwanao na utayari wako kumwelekeza kukitumia ili kiweze kumnufaisha badala ya kumharibu,” aliongeza.

Aina tofauti za teknolojia zitawafaa watoto wa umri tofauti. “Mtoto wako anaweza kuanza kwa kujua kupiga simu. Kisha ajifunze kutuma na kuandika arafa fupi (SMS). Baadaye anakomaa na kuanza kutumia Apu tofauti. Muhimu ni kukumbuka kwamba katika masuala haya ya teknolojia, watoto wana viwango tofauti vya ukomavu,” aeleza Dkt Amanda.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*