MKUTANO ambao ulikuwa umeitishwa na Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Uwiano kusuluhisha mgogoro kati ya Gavana Kawira Mwangaza na Bodi ya Ajira ya Kaunti ya Meru (CPSB), jana ulikosa kufikia malengo yake.
Gavana Mwangaza yupo kwenye mzozo mkali na na bodi hiyo kuhusu mpango wa kuwaajiri wafanyakazi zaidi ya 500.
Mapema mwaka huu CPSB ilitangaza nafasi hizo za kazi lakini Bi Mwangaza akasema hazipo na hata tangazo la uwepo wa kazi zenyewe lililowekwa kwenye mtandao wa kaunti likaondolewa.
Katibu wa Kaunti, Kiambi Atheru, baadaye alichapisha tangazo kwenye magazeti akisema kazi hizo hazipo lakini Afisa Mkuu Mtendaji wa CPSB, Bi Virginia Kawira, akasema mchakato wa uajiri utaendelea.
Madiwani pia waliingilia kati na kumshutumu gavana kuhusu kusitisha shughuli naye Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC), ikisema kuwa uajiri huo ulikuwa ukienda kinyume na agizo la Mdhibiti wa Bajeti (CoB).
Jana, Seneta wa Marsabit Mohamed Chute kwenye kikao, aliichemkia mirengo hiyo miwili kwa kukosa kuelewana na hata kushauriana na seneti kuhusu suala hilo tata.
Bw Atheru alichemkiwa na kulazimishwa kuomba msamaha kuhusu kauli aliyotoa hapo awali kuwa bodi hiyo ilikuwa na wanachama ambao walikuwa wamebobea kwenye ufisadi.
Bi Mwangaza naye alikuja juu na kulalamika kuwa Naibu Spika wa Bunge la Kaunti Mwenda Ali alikuwa akimdharau akisema walikuwa wakishinikiza uajiri uendelee ilhali uongozi wa kaunti umekataa.
Mwishowe pande zote hazikuelewana, zikiendelea kushikilia msimamo mkali kuhusu uajiri wa wafanyakazi 500.
Leave a Reply