KIWANDA cha kutengeneza sukari cha Sony katika Kaunti ya Migori wikendi kilirejelea shughuli zake baada ya kufungwa kwa wiki mbili ili kurekebisha mitambo yake.
Urekebishaji huo uligharimu Sh300 milioni na ulilenga kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinaendesha operesheni zake kikamilifu bila mitambo kuharibika kila mara.
Hitilafu hizo za kimitambo zimekuwa na athari kubwa za kifedha kwa kiwanda hicho cha sukari.
“Mitambo hiyo ilikuwa katika hali mbaya na kufanya iwe vigumu kwa kiwanda kutimiza malengo yake, jambo ambalo limetusababishia hasara tele,” akasema Meneja Mkurugenzi Martine Dima.
Bw Dima alisema kuwa wanatarajia marekebisho hayo yatapiga jeki shuguhuli ziendelee kwa angalau miezi sita mfululizo bila tatizo lolote.
Alifichua kwamba kiwanda hicho kitafungwa tena Mei 2025 ili kufanyiwa ukarabati wa kina ikiwemo kuondoa kabisa mitambo ya zamani na kuweksa mipya.
Afisa mkuu huyo alieleza kwamba mitambo ya zamani haikuwa imerekebishwa au kubadilishwa kwa miezi 12 ndiposa kiwanda hicho hakikuwa kinatimiza viwango vya uzalishaji.
Baada tu ya kuteuliwa kama mkurugenzi wa Sony mnamo Mei 2024, Bw Dima aliweka kipaumbele mipango ya kutunza rasilimali na kuongeza kiwango cha uzalishaji ili kukatiza mtindo wa kutegemea ufadhili wa serikali kwa kila jambo katika operesheni zzao.
Kiwanda hicho kilianzishwa mnamo 1978 na kinastahili kusaga tani 3,000 za miwa kila siku. Hata hivyo, kimeandamwa na changamoto tele ikiwemo hitilafu za mitambo, ambao umedidimiza usagaji miwa.
Huku akikiri kuwa changamoto zinazonga kiwanda hicho bado ni nyingi, Bw Dima alikuwa na imani kwamba ukarabati wa kina ambao wamepanga kutekeleza mwakani utaimarisha sio tu mapato ya kampuni bali pia ya wakuzaji miwa.
“Shughuli hizi za ukarabati zinalenga kuhakikisha operesheni za kiwanda zinaendelea bila tatizo na kurejesha matumaini kwa wakulima na washikadau wa miwa katika ukanda huu kwamba kilimo cha miwa kina natija,” akasema.
Meneja huyo mkurugenzi alihimiza wakulima wa hapo kuongeza kiwango cha ekari wanakokuza miwa ili kiwanda kiwategemee badala ya kununua zao hilo kutoka maeneo mengine na hivyo kutatizikia gharama ya usafiri.
Kampuni ya Sony ina ekari 2,400 za ardhi ambako kinakuza miwa japo pia wakulima wa kibinafsi wanakuza miwa katika ekari nyingine 6,000 na kuwasilisha katika kiwanda hicho.
Vile vile, Bw Dima alisema uamuzi wa kulipa wakulima kwa wakati au hata mapema kumewapa motisha wakuzaji ambao walikuwa wameasi kilimo hicho na sasa wamekirejelea.
“Sasa tunapokea tani 20,000 za miwa kila wiki, idadi ambayo ni ya juu kuliko zamani,” akaongeza.
Hata hivyo, kikwazo kikuu kwa Sony Sugar deni la Sh800 milioni la wafanyakazi ambalo limerundikana kwa miezi 16 iliyopita.
Leave a Reply