Kamworor kutafuta michuzi Barcelona Half Marathon na Rotterdam Marathon – Taifa Leo


MSHIKILIZI wa zamani wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 21, Geoffrey Kamworor, amethibitisha kutafuta michuzi ya mbio za Barcelona Half Marathon nchini Uhispania hapo Februari 16 na pia Rotterdam Marathon nchini Uholanzi mnamo Aprili 13.

Kamworor alishinda Copenhagen Half Marathon kwa rekodi ya dunia dakika 58 na sekunde moja mnamo Septemba 15, 2019 ambayo ilivunjwa na Kibiwott Kandie akitawala Valencia Half kwa 57:32 mnamo Desemba 2020.

Rekodi hiyo iliimarishwa na Mganda Jacob Kiplimo katika Lisbon Half (57:31) mwaka 2021 na kisha Muethiopia Yomif Kejelcha (57:30) mwaka jana. Kiplimo pia ametoa ithibati ya kushiriki Barcelona Half bila kusahau Roncer Konga (59:08).

Joyciline Jepkosgei akikata utepe kutwaa ubingwa wa Barcelona Half Marathon nchini Uhispania, kwa rekodi ya dunia ya awali. PICHA | MAKTABA

Kitengo cha kinadada cha Barcelona Half kimevutia mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia Joyciline Jepkosgei (saa 1:04:29), Gladys Chepkurui (1:05:46) na Nancy Sang (1:06:52). Jepkosgei anajiandaa kutimka mbio za kilomita 42 za London Marathon nchini Uingereza mwezi Aprili.

Kamworor anayejivunia muda bora wa 2:04:23 katika mbio za 42km, atapimwa vilivyo na Mbelgiji Bashir Abdi (2:03:36) mjini Rotterdam.

Amos Kipruto na Philemon Kiplimo nao wameingia Haspa Hamburg Marathon nchini Ujerumani hapo Aprili 27. Kipruto alishinda London Marathon mwaka 2022.

Waethiopia Guye Adola na Kinde Atanaw ni baadhi ya wakimbia matata ambao Wakenya watalazimika kukabiliana nao ili kushinda mjini Hamburg.

Nao Erick Sang na Emily Chebet wataonyesha talanta zao kwenye mbio za Loop Den Haag Half Marathon nchini Uholanzi hapo Machi 9.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*