Kandarasi yangu na Ruto imeisha – Taifa Leo


ALIYEKUWA rais wa Baraza la Mawakili Nchini (LSK), Nelson Havi ameongeza uzito kwenye azma ya Jaji Mkuu (CJ) Mstaafu David Maraga kumenyana na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Havi, Jumanne asubuhi, Februari 11, 2025 kwenye mdahalo na runinga ya Citizen alisema kandarasi yake na Dkt Ruto imeisha.

Alisema, ulikuwa mkataba wa miaka mitano pekee na hatarajii kuutekeleza upya.

Rais huyo wa zamani LSK, katika uchaguzi mkuu wa 2022 aliunga mkono kuchaguliwa kwa Rais Ruto.

Bw Havi alikuwa mwanachama wa United Democratic Alliance (UDA), chama kinachoongozwa na Rais Ruto.

“Kandarasi yangu na Dkt William Samoei Ruto ilikuwa ya miaka mitano. Na miaka mitano inapoelekea kukamilika, sitarajii kufanya upya mkataba mwingine naye,” Bw Havi alisema.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, rais huyo wa zamani LSK aliwania kiti cha ubunge Westlands, Nairobi kupitia tikiti ya UDA.

Alimenyana na mbunge wa sasa Bw Timothy ‘Tim’ Wanyonyi aliyefanikiwa kuwania kuhifadhi chake kwa chama cha ODM.

Bw Wanyonyi, ambaye ni mwandani wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga, aliibuka mshindi kwa kuzoa kura 58,400 kulingana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), naye Havi akimfuata kwa kura 19,500.

Bw Havi ameweka wazi kuwa anaunga mkono CJ Maraga kutoana kijasho na Rais Ruto 2027, akipambana kuhifadhi kiti chake kwa muhula wa pili na wa mwisho.

“Ninasema tunapaswa kuwa na David Kenani Maraga kama Rais ajaye wa Jamhuri ya Kenya,” Havi akasema.

Bw Havi alisisitiza kwamba hayo ni maamuzi yake, na hakuna atakayemkosoa.

“Hakuna aliyeniwekea bima,” alihoji.

Bw Havi alidai yeye huongea ukweli na kwa niaba ya Wakenya, hivyo basi taifa halina budi ila kufanya jambo linalofaa.

Bw Maraga na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i ni kati ya vigogo ambao wametajwa uwezekano wao kuwepo debeni 2027 kumenyana na Rais Ruto.

Baadhi ya viongozi na wanasiasa, wamejitokeza na kupigia debe wawili kumrithi Ruto.

Bw Maraga anakumbukwa kutokana na maamuzi yake 2017 kufutilia mbali ushindi wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, hatua iliyoshinikiza taifa kushiriki uchaguzi mwingine kiti cha urais.

Bw Kenyatta alikuwa akishindana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*