MPANGO wa serikali ya Kaunti ya Murang’a wa kuboresha utoaji wa huduma za afya bila malipo kwa wanajamii wanaotaabika kulipia ada hizi maarufu Kang’ata care, umeshinda tuzo ya mradi bunifu zaidi unaohudumia umma barani Afrika.
Kang’ata Care ilibwaga miradi 68 kutoka serikali mbalimbali za nchi za Afrika zikiwemo Mauritius, Misri, Tanzania, Zambia na Uganda ambazo zilifika katika hatua ya fainali ya mashindano hayo.
Tuzo hii inayotathmini programu za kuhudumia umma katika mataifa 55 barani, hutolewa na Shirika la Afrika la Usimamizi wa Miradi ya Umma (AAPAM).
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata alisema ushindi huu ni motisha wa kuzidisha ari ya kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Vile vile, alitaja kutambuliwa huku kuwa fahari sio tu kwa jumuiya ya Murang’a, pia kwa taifa zima.
“Tumeshinda tuzo hii kwa niaba ya Wakenya wote wala si wakazi wa Murang’a pekee. Ninatoa shukurani kwa watumishi wa umma waliobuni wazo hili na pia bunge la kaunti kwa kupitisha mpango huu pamoja na kuendelea kutoa bajeti ya kuusimamia uwe endelevu,” akasema Bw Kang’ata baada ya kutawazwa mshindi.
Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma Amos Gathecha alimpongeza Gavana Kang’ata kwa kubuni mradi huu kwa watu wasiojiweza katika jamii.
“Amekuwa akiangazia maslahi ya watu ambao wako katika ngazi ya chini ya kiuchumi. Yeye hutumia pesa anazopata kutoka kwa mapato ya kaunti na ya serikali kuu kuwashughulikia wasiojiweza,” akasema Bw Gathecha.
Rais wa AAPAM Dkt John Nakabago alipongeza Kenya na kusisitiza umuhimu wa tuzo hizi.
“Tunatambua taasisi ambazo zinabadilisha maisha ya wananchi sio tu Afrika, bali pia nje ya bara,” alieleza.
Si mara ya kwanza Kenya kutambuliwa. Mpango wa vituo vya huduma – Huduma Centre – uliwahi kutuzwa baada ya kuibuka namba mbili mnamo mwaka wa 2022.
Pia, hatua ya serikali kuhudumia wananchi kupitia mitandao wa e-citizen ili kurahisisha utekelezaji wa mipango ya serikali ilitambuliwa moja ya programu bunifu mwaka wa 2017.
Leave a Reply