Kanisa la ‘Bethel for Jesus’ Bomet linalochoma na kuangushia kipigo waumini – Taifa Leo


POLISI katika Kaunti ya Kericho wameanzisha uchunguzi kuhusu kanisa tata la Bethel for Jesus Ministry International linaloshutumiwa kwa vitendo vyake vya kikatili baada ya kujaribu kumteketeza ajuza mmoja kutoka kijiji cha Kapkatet.

Bi Mercy Cherotich, alimtembelea binamu yake ambaye alimwalika ahudhurie ibada katika kanisa hilo lililoko mji wa Kapkwen mnamo Februari 19, 2025.

Hata hivyo, masaibu ya Bi Cherotich yalianza alipokataa kufika mbele ya washirika wengine.

“Niliwaambia siwezi kwenda mbele kwa sababu mimi si mshiriki wa kanisa hilo na sikujua kilichokuwa kinatarajiwa kwangu. Mchungaji alinipiga kofi mara mbili huku mashemasi wakimkabidhi fimbo ambayo alitumia kunichapa mwili mzima,” Bi Cherotich akasema.

Alisema kuwa alielezwa kuwa kipigo hicho kilikuwa cha ‘kutoa mapepo’ yaliyokuwa ndani yake.

Baadaye aliwasilisha ripoti katika Kituo cha Polisi cha Kapkwen chini ya OB 12/19/02/2025. Uchunguzi wa kimatibabu ulithibitisha kuwa alipata majeraha mgongoni, miguuni na mikononi.

“Nataka wachungaji wawajibike kwa walichonitendea,” alisema Bi Cherotich, akiwa na mshtuko kutokana na masaibu aliyoyapitia.

Tukio hilo limefufua kumbukumbu ya video ya kutisha ya 2024 ambayo imeenea mitandaoni, ikionyesha ajuza akionekana amefungwa na kuchomwa moto hadharani nje ya kanisa.

Kwenye video hiyo, alisikika akipiga mayowe akiomba msamaha huku akiahidi kutubu na kujiunga na kanisa hilo. Lakini watu waliomteka walikataa na kuendelea kumsogeza juu ya moto ulio wazi.

“Aliendelea kuomba maisha yake yaokolewe, lakini walimpuuza,” alisema mkazi mmoja aliyeshuhudia tukio hilo.

Ufichuzi huo ulisababisha mchungaji mkuu wa kanisa na wasaidizi wake 15 kuingia mafichoni. Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Chepalungu Phantom Nalo, alisema angalau waathiriwa wawili wameandikisha taarifa rasmi kwa polisi.

Bw Nalo alisema mlalamishi mmoja kutoka Kanusin aliandikisha taarifa Februari 12, 2025, kuhusu jinsi pasta alimwita na kumchapa kwa fimbo.

“Alipata majeraha mwili mzima na alifanikiwa kutoroka kanisani,” ilisema ripoti ya polisi.

Kuhusu kisa cha Bi Cherotich, ripoti inasema alitembelea kanisa hilo na wakati mchungaji alipokuwa akihubiri, aliruka kutoka mimbari na kuamwangusha chini.

“Alimcharaza viboko vikali, hivyo kumsababishia majeraha ya mwili.”

Jana Bw Nalo alisema waathiriwa wote wawili walipewa fomu za matibabu (P3) nao polisi walitembelea eneo la tukio kutafuta ushahidi.

“Polisi wametembelea eneo hilo na uchunguzi zaidi unaendelea. Watuhumiwa, akiwemo mchungaji Zachary, wako mafichoni na wanatafutwa na polisi,” akasema Bw Nalo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*