Katibu Kiptoo hatarini kukamatwa kuhusiana na kupunguza Sh100 milioni za Inua Jamii – Taifa Leo


BUNGE limetoa agizo kumshinikiza Katibu wa Wizara ya Fedha Chris Kiptoo kufika mbele ya kamati ya Bunge kueleza sababu za kupunguza zaidi ya Sh100 milioni za mpango wa Inua Jamii.

Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Ulinzi wa Kijamii ilitumia Kifungu cha 125 cha Katiba kumshinikiza Dkt Kiptoo kufika mbele yake baada ya kususia mialiko mitatu.

Dkt Kiptoo sasa anakabiliwa na hatari ya kukamatwa na kuwasilishwa bungeni au kutozwa faini ya Sh500,000 iwapo atakosa kuheshimu wito huo.

“Tuliitisha mkutano ambao haukufanyika Ijumaa iliyopita kwa sababu Dkt Kiptoo hakufika. Tuliahirisha kikao hadi Jumatano Desemba 4, 2024 lakini tena Katibu hayupo kujadili suala hili muhimu sana la kupunguzwa kwa bajeti ya Inua Jamii,’’ Alice Ng’ang’a, ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo alisema.

“Kwa sababu Katibu ameamua kututumia afisa tuliyemrudisha Ijumaa iliyopita Bw Johnah Wala, Mkurugenzi wa Hazina ya Huduma za Uhasibu, bila maelezo yoyote, kamati imeamua kutumia kifungu cha 125 cha Katiba na Kanuni ya Kudumu ya 131 kuagiza Katibu wa Wizara ya Fedha kufika mbele ya kamati hii. Kikao hiki kimeahirishwa,’’ alisema mwenyekiti huyo.

Kamati hiyo haikutaja tarehe ambayo Dkt Kiptoo anatakiwa kuheshimu agizo hilo lakini ilisema itataja tarehe na saa katika agizo.

Dkt Kiptoo, kama alivyofanya Ijumaa iliyopita, alimtuma Bw Wala kumwakilisha katika kikao ambacho pia kilihudhuriwa na Katibu wa Ulinzi wa Jamii na Huduma za Wazee Joseph Motari.

Dkt Kiptoo alitarajiwa kueleza kamati hiyo sababu za kupunguzwa kwa zaidi ya Sh100 milioni zilizokusudiwa mpango wa Inua Jamii.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*