MIAKA 12 iliyopita, Titus Ngamau almaarufu Katitu, alikuwa afisa wa polisi aliyeogopwa sana.
Leo, Katitu hutegemea sana mapato kutoka kwa bendi yake ya Kithangaini Lipua Lipua akijaribu kujenga upya maisha yake baada ya kuachiliwa kutoka Gereza Kuu la Kamiti, ambako alifungwa kwa miaka sita.
Maisha yalibadilika mnamo 2013 baada ya kumpiga risasi Kenneth Kimani, ambaye afisa huyo wa polisi alidai alikuwa mshukiwa wa uhalifu huko Githurai, hatua ambayo ilimtumbukiza katika mfululizo wa matukio ambayo yalisababisha kufungwa kwake 2018 baada ya Jaji James Wakiaga kumpata na hatia ya kutumia vibaya silaha.
Baada ya kuachiliwa huru miezi miwili iliyopita, Katitu aligeukia muziki wa benga ili kujikimu kimaisha. Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 51, mtunzi wa nyimbo na mpiga gitaa anategemea bendi ya muziki ambayo wanachama wake wakuu ni watoto wake.
“|Ni mwanangu ambaye alinitambulisha kwa wateja wangu wengi wa sasa,” aliambia Taifa Leo akimzungumzia mwanawe mkubwa Mwaniki ‘Kitolongwe’ Ngamau, 25, ambaye aliongoza bendi babake alipokuwa gerezani.
Elizabeth Mumbua, 23, ni mwimbaji na anapiga gitaa la rithimu huku Pius Kivuva, 21, akipiga gitaa la bezi na solo kando na kuwa mwimbaji. Michael Kasyoki, mzaliwa wa mwisho ambaye alisherehekea miaka 18 ya kuzaliwa Juni, anacheza gitaa la bezi.
“Muziki uko katika damu ya familia yetu,” Katitu anasema.Katitu anasema alirithi kipawa chake cha muziki kutoka kwa babake, Peter Musila, ambaye alikuwa mwanamuziki mashuhuri wa benga Ukambani akiongoza Bendi ya Kithangaini Brothers miaka ya 1970.
Afisa huyo wa polisi wa zamani anaweza kuwa na hamu ya kuimba wimbo mpya katika maisha yake, lakini kivuli cha maisha yake ya zamani linamwandama.
Miaka saba baada ya kuhukumiwa, Katitu amesalia kuwa kipenzi kwa baadhi ya watu kwa mbinu zake za kukabiliana na uhalifu huku wengine wakimchukulia kuwa mhalifu.
Hata hivyo, anasitasita kuzungumzia jambo hilo, akiahidi bila kufafanua kwamba atafunguka wakati ufaao.’Tusilizungumzie hilo sasa,’ aliambia Taifa Leo alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwake, kushtakiwa na hatimaye kusukumwa jela.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply