KAUNTI hatari kwa ufujaji wa pesa za umma huenda zikaorodheshwa na kuanikwa ikiwa Seneti itatekeleza tishio lake la kuhakikisha matumizi bora ya fedha.
Haya yaliibuka huku maseneta wakiwasuta magavana kuhusu matumizi mabaya ya pesa za walipa ushuru wakati wa kikao cha siku mbili cha kutathmini utendakazi wa Seneti katikati ya muhula na kujipanga kwa Kikao cha Nne.
Naibu Spika wa Seneti Kathuri Murungi, alizitaka kamati za Seneti kuanza kuorodhesha na kufichua majina ya kaunti ambazo zimejizolea sifa mbaya kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.
Alisema kwamba hatua hii itaimarisha uwajibikaji.
“Kuna haja kamati za Seneti zinazoshughulikia ripoti zilizokaguliwa, kutambua na kuwasilisha katika Seneti kaunti zinazoongoza kwa ufujaji wa fedha uliokithiri. Ufichuzi kama huo utawapa Wakenya uwezo wa kudai uwajibikaji na kulinda haki zao,” akasema Bw Murungi.
“Wakenya wamekuwa wakitafuta taarifa kuhusu kaunti ambazo fedha zinatumiwa vibaya. Bunge la Seneti kupitia kamati zake, linafaa kuwa na uwezo wa kufanya hivyo ili magavana wachukuliwe hatua kuhusiana na matumizi mabaya ya fedha na ikiwezekana warejeshe pesa hizo,” aliongeza Bw Murungi.
Seneta huyo wa Meru pia alisisitiza jukumu la uangalizi la Seneti akisisitiza umuhimu wa uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma.
“Moja ya majukumu yetu kama Seneti ni usimamizi. Tunapaswa kuwa na orodha ya kaunti ambazo pesa zinafujwa ili tuulize maswali mazito na kuhakikisha rasilimali zinatumiwa vyema,” alisema.
Matamshi ya Seneta Murungi yanajiri kukiwa na wasiwasi kuhusu ubadhirifu wa fedha katika kaunti kadhaa, huku ripoti zikionyesha visa vya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Magavana, maspika wa mabunge ya kaunti, makarani na wawakilishi wa wadi (MCAs) katika baadhi ya kaunti, wameshutumiwa kwa kushirikiana kuiba pesa za umma.
Ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu na Mdhibiti wa Bajeti (CoB), Bi Margaret wa Nyakang’o, zimefichua matumizi mabaya ya fedha.
Mnamo Januari 28, 2025, EACC ilifichua kuwa jumla ya kaunti 11 zinachunguzwa kuhusiana na madai ya kutumia vibaya pesa za umma.
Leave a Reply