RIPOTI ya Mdhibiti wa Bajeti (COB) imeonyesha kuwa kaunti zinatumia asilimia 70 za bajeti zao katika ulipaji mishahara na kuibua wasiwasi kuhusu mgao unaoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa COB kaunti zilitumia Sh38.69 bilioni kulipa mishahara ndani ya miezi mitatu hali hii ikionyesha kuwa kaunti zina wafanyakazi wengi na huenda kuna mgongano wa majukumu.
Takwimu za robo ya kwanza ya mwaka wa fedha unaokamilika Juni 30, 2025 zilionyesha kuwa kaunti zimetumia Sh55.68 bilioni ambapo Sh48.96 bilioni zimelipa mishahara na kuelekezwa kwenye matumizi mengine ya afisi.
Ni Sh6.71 bilioni pekee ndizo zilielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Kinachoshangaza ni kuwa kaunti 10 hazikutumia hela zozote kwa miradi ya maendeleo kwenye kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Kaunti hizo ni Baringo, Elgeyo-Marakwet, Kajiado, Kisii, Lamu, Nairobi, Nyandarua, Tana River, Uasin Gishu na Pokot Magharibi.
Kaunti hizo 10 zilitumia Sh7.48 bilioni kulipa misharahara ya wafanyakazi Nairobi ikiongoza kwa Sh2.57 bilioni, Kisii (Sh876.8 milioni), Kajiado (Sh844.4 milioni), Uasin Gishu (Sh798.6 milioni), Elgeyo Marakwet (Sh616.3 milioni), Pokot Magharibi (Sh486.1 milioni), Baringo (Sh448.9 milioni), Tana River (Sh303. Milioni), Lamu (Sh282.3 milioni) na Nyandarua (Sh255.1 milioni).
Mnamo Novemba 2023, Ripoti ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) iliwaweka idadi ya wafanyakazi wa kaunti kuwa 184,876 huku Nairobi ikiwa na wafanyakazi 13,513.
Kakamega ilifuata kwa wafanyakazi 7,087, Bungoma (6,477), Kisii (5,965), Machakos (5,777), Mombasa (5,739) na Nakuru (5,681).
Ripoti ya COB inasema kaunti zote 47 kwa sasa inawaajiriwa wapya 67, 974 ambao walipata kazi kati ya 2016-2023. Huenda idadi hiyo ikapanda zaidi kwa kuwa Kaunti ya Garissa haikuwasilisha takwimu zake.
“Hii inaonyesha kuwa kaunti kadhaa huenda hazina chochote baada ya kuwalipa wafanyakazi mishahara,” akasema Mwenyekiti wa kamati ya Uhasibu katika Bunge la Seneti Moses Kajwang’ ambaye pia ni seneta wa Homa Bay.
Hata hivyo, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (COG) Mutahi Kahiga amesema kuna hitaji kubwa la huduma kwenye sekta za afya na elimu ndiposa idadi ya wafanyakazi imekuwa ikipanda.
Bw Kahiga alisema elimu ya chekechea na katika vyuo vya kiufundi iligatuliwa lakini hazikutengewa fedha.
Baadhi ya magavana nao wamekuwa wakilalamika kuwa walirithi wafanyakazi wengi kutoka kwa zilizokuwa serikali za mitaa huku pia wakilaumu serikali kuu kwa kuchangia ongezeko la wafanyakazi katika kaunti.
Leave a Reply