KCSE ya mwisho ni 2027, KNEC yatangaza – Taifa Leo


MTIHANI wa mwisho wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) utafanywa mwaka wa 2027, Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC) David Njeng’ere ametangaza.

Akiongea Alhamisi katika shughuli ya kutolewa kwa matokeo ya KCSE 2024, Bw Njeng’ere alisema kuwa hatua hiyo ndio itakuwa mwisho wa mfumo wa elimu wa 8-4-4 na kukumbatiwa kikamilifu kwa mtaala mpya wa Umilisi na Utendaji (CBC).

“Ningependa kujulisha umma kwamba KCSE ya mwisho itafanywa mwaka wa 2027. Kwa hivyo, ningependa kuwaalika wale ambao wangetaka kurudia KCSE kufanya hivyo ndani ya nafasi tatu zilizosalia,” akaeleza katika Makao Makuu ya Baraza la KNEC, Nairobi

Bw Njeng’ere, pia, alitangaza kuwa wanafunzi waliojiunga na Gredi 9 mwaka huu, 2025, watafanya Mtihani wa Kenya Junior Secondary Education Assessement (KJSEA).

“Tulifanya majaribio ya mtihani huo Julai mwaka jana (2024) kwa jumla ya shule 235 katika kaunti zote 47,” akasema afisa huyo.

Bw Njeng’ere alisema kuwa karatasi za majaribio ya mtihani wa KJSEA ziko tayari na zinapatikana katika mtandao wa KNEC.

“Karatasi hizo zinapatikana bure na wananchi wasikubali kuuziwa na watu wakora,” akatahadharisha.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*